IQNA

Jinai za Israel

Mahakama ya Kimataifa yauamuru utawala wa Israel usitishe hujuma dhidi ya Rafah huko Gaza

6:23 - May 25, 2024
Habari ID: 3478881
IQNA-Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imeutaka Utawala wa Kizayuni wa Israel usitishe mashambulizi yake katika mji wa kusini wa Gaza wa Rafah na kujiondoa katika eneo hilo, katika kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini ikiishutumu Israel kwa kufanya mauaji ya kimbari, na kuielezea hali hiyo kuwa ni hatari kubwa kwa wakazi wa Palestina.

Uamuzi huo wa Ijumaa wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) umekuwa ni wa tatu kutolewa mwaka huu na jopo la majaji 15 ambalo limetoa maagizo ya awali ya kutaka kudhibitiwa ongezeko la idadi ya vifo na kupunguza mateso ya kibinadamu huko Gaza.

 Ingawa amri za ICJ zina nguvu kisheria, lakini mahakama hiyo haina vyombo vya kulazimisha utekelezaji wake. Akisoma uamuzi huo wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki au Mahakama ya Dunia,

Rais wa Jopo la Majaji, Nawaf Salam, amesema hatua za muda zilizoamriwa na mahakama hiyo mwezi Machi hazijashughulikia kikamilifu hali ya eneo la Palestina linalozingirwa hivi sasa, na hali ya sasa imeweza kuzingatiwa ipasavyo kwa agizo jipya la dharura lililotolewa.

Jaji Salam amesema Israel lazima ikomeshe mara moja mashambulizi yake ya kijeshi, na hatua nyingine yoyote katika eneo la Rafah, ambayo inaweza kusababishia kundi la Wapalestina huko Gaza hali ya maisha ambayo inaweza kuleta uharibifu wa kimwili kwa ujumla wao au kwa baadhi yao; na kuielezea hali ya kibinadamu katika mji wa Rafah kuwa ni mbaya.

Wiki iliyopita, Mawakili wa Afrika Kusini waliitaka mahakama ya ICJ yenye makao yake mjini The Hague kuchukua hatua za dharura, wakisema mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Rafah lazima yakomeshwe ili kuhakikisha usalama wa maisha ya Wapalestina.

Baada ya Harakati ya Hamas kutekeleza operesheni ya Kimbunga cha Aqsa tarehe 7 Oktoba kulipiza kisasi jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina,  jeshi la utawala huo ghasibu wa Israel lilianzisha vita vya mauaji ya kimbari na hadi sasa limeshaua shahidi Wapalestina 35,709 katika Ukanda wa Gaza na kuwajeruhi wengine 79,990, wengi wakiwa ni wanawake na watoto

3488474

Habari zinazohusiana
captcha