IQNA

Jinai za Israel

Jeshi katili la Israel laua Wapalestina 210 katika 'hujuma ya kinyama' kwenye kambi ya Nuseirat

10:38 - June 09, 2024
Habari ID: 3478951
IQNA-Idara ya Habari ya Serikali ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza imesema, askari wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel wamefanya "shambulio la kikatili ambalo halijawahi kushuhudiwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Nuseirat" na kuua kwa umati Wapalestina 210 hadi hivi sasa na makumi ya watu kujeruhiwa mitaani.

Taarifa iliyotolewa na Idara hiyo leo imeeleza kwamba jeshi la Kizayuni linaendeleza uchokozi wake dhidi ya maeneo yote ya Jimbo la Kati la Deir el-Balah; na hali katika Hospitali ya Mashahidi wa Al-Aqsa ni mbaya sana.
 
Kwa mujibu wa idara hiyo ya habari, vikosi vya jeshi la Kizayuni vimeanzisha "uvamizi wa kinyama na wa kikatili" katika kambi hiyo, vikiwalenga raia moja kwa moja na kwamba magari ya kubebea wagonjwa na wafanyakazi wa ulinzi wa raia hawawezi kufika eneo hilo kutokana na ukubwa wa mashambulizi ya mabomu.
 
Ofisi hiyo imetahadharisha kuwa Hospitali ya Mashahidi wa Al-Aqsa ndiyo pekee inayofanya kazi katika eneo la Deir el-Balah, tena kwa jenereta moja tu la umeme; na kwamba ikiwa jenereta hilo pekee litasita kufanya kazi "maafa halisi" yatatokea.

Taarifa ya idara hiyo imeendelea kueleza: "hospitali hii inatoa huduma za afya kwa watu milioni moja na watu waliolazimika kuhama makazi yao, na haiwezi kuhudumia idadi hii kubwa ya waliouawa shahidi na majeruhi".

 
Idara ya Habari ya Serikali ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza imetoa wito kwa Jamii ya Kimataifa, Umoja wa Mataifa na mashirika yote ya kimataifa "kuingilia kati mara moja na kwa haraka kuokoa hospitali hiyo na kuokoa hali ya afya katika eneo hilo la katikati mwa Ghaza.
 
Taarifa hiyo imeeleza bayana kwamba, inalibebesha jeshi vamizi la Israel na serikali ya Marekani dhima kamili ya jinai hiyo ya kutisha ya kumwagwa damu za makumi ya raia wasio na hatia katika eneo hilo.
3488670
 
Habari zinazohusiana
Kishikizo: jinai za israel
captcha