IQNA

Jinai za Israel

Israel yaua shahidi Wapalestina kadhaa katika hujuma ya kinyama dhidi ya kambi ya Jenin

17:32 - July 03, 2023
Habari ID: 3477233
JENIN (IQNA)- Jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel limefanya mashambulizi ya kinyama ya anga kwenye kambi ya wakimbizi ya Jenin katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na kuua shahidi Wapalestina wasiopungua wanane na kujeruhi makumi kadhaa.

Wakazi wa eneo hilo pamoja na maafisa wa Palestina wamesema, Wapalestina wasiopungua saba wameuawa shahidi na wengine wasiopungua 27 wamejeruhiwa hadi sasa kutokana na mashambulio hayo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, Mpalestina wa nane, Mohammad Hasanein mwenye umri wa miaka 21, aliuawa usiku wa kuamkia leo Jumatatu na jeshi la utawala wa Kizayuni kwenye lango la kaskazini la mji wa Ramallah katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Mashuhuda wamevieleza vyombo vya habari kuwa jeshi la utawala dhalimu wa Israel limefanya mashambulizi 10 ya anga mjini Jenin usiku wa kuamkia leo na kusababisha moshi kufuka kutoka kwenye mabaki ya majengo.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa msafara wa makumi ya magari ya kivita ya Israel pia yalizingira kambi ya wakimbizi ya Jenin na kuanzisha operesheni ya kijeshi ya ardhini, na kusababisha uharibifu mkubwa kwa nyumba na barabara.

Kwa mujibu wa duru za habari, magari ya kivita 150 na askari wapatao 1,000 wa vikosi maalumu vya jeshi la utawala wa Kizayuni, vya intelijensia, polisi na polisi wa mpakani wameshiriki katika operesheni hiyo.

Wakati huohuo, Wizara ya Afya ya Palestina imetaja majina ya watu wanne kati ya waliouawa huko Jenin kuwa ni Sameeh Abu al-Wafa, Hussam Abu Theeba, Aws al-Hanoun na Nour el-Din Marshoud, ikibainisha kuwa wote hao walipigwa risasi kifuani na kichwani.

Taarifa ya wizara hiyo imesema Wapalestina wengi waliojeruhiwa wako mahututi na kuongeza kuwa, idadi ya vifo inaweza kuongezeka sana kwa sababu mabuldoza ya jeshi la utawala wa Kizayuni yamefunga njia na kuwafanya watoaji huduma za tiba washindwe kuwafikia majeruhi.

Aidha imeripotiwa kwamba, sambamba na mashambulio ya jeshi la kizayuni, umeme katika mji wa Jenin umekatika.

Katika upande mwingine, vikosi vya Muqawama wa Palestina katika kambi ya Jenin vimefanikiwa kuziangusha ndege mbili zisizo na rubani za utawala wa Kizayuni katika anga ya kambi hiyo.

Kikosi cha wapiganaji wa Jenin chenye mfungamano na brigedi za Al-Quds kimetangaza leo kuwa vikosi hivyo vimefanikiwa kuziangusha ndege mbili zisizo na rubani za utawala haramu wa Israel.

4152036

Habari zinazohusiana
Kishikizo: jinai za israel jenin
captcha