IQNA

Uchambuzi kuhusu jinai za Israel

Jitihada za kukabiliana na jinai za kibaguzi za Israel

20:44 - June 11, 2023
Habari ID: 3477135
Mashirika mia moja ya Kimarekani yameanzisha mpango uliopewa jina la "Jamii Zisizo na Ubaguzi wa Rangi" kwa lengo la kusitisha uungaji mkono wa nchi yao kwa utawala wa kibaguzi wa Israel.

Taarifa iliyotolewa na mashirika mia moja ya Kimarekani kuhusu kampeni ya "Jamii Zisizo na Ubaguzi wa Rangi" imesema kwamba mpango huo unalenga kuanzisha vuguvugu huko Amerika Kaskazini la kukomesha ubaguzi wa rangi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Taarifa hiyo imetoa wito wa kuanzishwa jamii huru zisizo na utawala wa ubaguzi wa rangi (apartheid) kwa kuepuka kuunga mkono utawala wa Israel, ambao ni utawala ghasibu na ukoloni wa walowezi.

Kadhalika imesisitiza azma ya kampeni hiyo ya kupigania uhuru, uadilifu na usawa kwa taifa la Palestina na watu wote na kupambana na aina zote za ubaguzi wa rangi na ukandamizaji.

Taarifa hiyo imesema, taifa la Palestina linakabiliwa na ukoloni, kukaliwa kwa mabavu ardhi yake na ujenzi wa vitoji vya walowezi unaofanywa na utawala wa Kizayuni kwa miongo kadhaa, wametwishwa sheria za kibaguzi, kulazimishwa kuyahama makazi yao, kuzingirwa, kuwekewa vizuizi vya kutembea na ukiukwaji uliopangwa wa haki za binadamu.

Taarifa ya mashirika mia moja ya Marekani imewanukuu watafiti wa sheria na jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu zikisema, "hali hii ni ukiukwaji wa sheria, na kwa msingi huo, tunataka kukomeshwa kwa utawala wa kibaguzi wa Israel."

Tarehe 25 Julai mwaka jana pia, kulianzishwa mpango kama huu uliopewa jina la "Pamoja Dhidi ya Apartheid" nchini Canada kwa lengo la kujenga utamaduni kwa Wacanada na kuwapa fursa ya kushiriki katika juhudi za kupambana na ukandamizaji unaofanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina.

Human Rights Watch ambalo ni shirika lisilo la kiserikali, la kimataiifa na lenye makao yake mjini New York Marekani Mei mwaka 2021 lilitoa ripoti ya kurasa 213 na kuitaja Israel kwamba, ni utawala wa ubaguzi wa rangi (apartheid) na ukaitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinaii kuwapandisha kizimbani viongozi wa Israel.

Kwa mujibu wa Human Rights Watch, baada ya miongo kadhaa ya maonyo ya mara kwa mara kuhusu uwezekano wa Israel kudhibiti maisha ya Wapalestina na kusababisha utawala wa kibaguzi, kizingiti hiki sasa kimevuka na hali ya sasa ni ya ubaguzi wa rangi.

Omar Shakir, mkurugenzi wa idara ya Israel na Palestina ya Human Rights Watch, akizungumzia utawala wa kibaguzi wa Israel, anasema: "Huu ni ugunduzi wa wazi zaidi ambao Human Rights Watch imefikia kuhusu tabia na mwenendo wa Israel wa miaka 30."

Kwa mujibu wa sheria za kimataifa hususan mkataba wa Roma ambao msingi wake ulipelekea kuanzishwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ubaguzi wa rangi unahesabiwa kuwa ni jinai dhidi ya binadamu.

Hatua za kinyama za Israel dhidi ya Wapalestina hazijaishia katika ubaguzi wa rangi (apartheid) bali utawala huo ghasibu umekuwa ukipora na kughusubu mtawalia ardhi za wananchi hao madhulumu katika maeneo mbalimbali ya ukingo wa magharibi wa Mto Jordan na kuzidi kupanua ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Si hayo tu, bali Israel ikitumia jeshi lake katili, imekuwa ikifanya hujuma na mashambulio ya kinyama katika Ukanda wa Gaza ambapo mbali na kufanya mauaji umekuwa ukiangamiza miundombinu yao sanjari na kubomoa nyumba zao. Kwa hakika hatua hizi za Israel ni vielelezo vya wazi vya jinai dhidi ya binadamu. Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za asasi na mashirika ya haki za binadamu likiwemo Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Israel inahesabiwa kuwa moja ya tawala zinazokiuka pakubwa haki za binadamu ulimwenguni.

 

Habari zinazohusiana
Kishikizo: jinai za israel
captcha