Swala ya Ijumaa imeswaliwa katika Msikiti wa Imam Muhammad ibn Abd al-Wahhab wa Doha ikifuatiwa na Swala ya Janaza ya Ismail Haniya.
Baada ya hapo mwili wa Shahidi Haniyeh, umesindikizwa na maelfu ya watu hadi kwenye makaburi ya kifalme ya Lusail kaskazini mwa Doha, ulikozikwa.
Haniya, ambaye alikuwa Tehran kuhudhuria hafla ya kuapishwa Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian, aliuawa pamoja na mlinzi wake, katika shambulio la kigaidi lililotekelezwa na utawala katili wa Israel kwenye makazi yake kaskazini mwa Tehran mapema Jumatano.
Siku ya Alkhamisi asubuhi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei aliuswalisha umati mkubwa wa Waislamu waliojitokeza katika Swala ya Maiti ya Ismail Haniya na mlinzi wake. Swala hiyo ya Maiti iliswaliwa katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Tehran.
Baada ya Swala hiyo, kulifanyika shughuli ya maziko kutoka kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Tehran na kuelekea katika Medani ya Uhuru na Ukombozi, mjini Tehran kabla ya mwili wa shujaa wa Palestina kupelekwa Doha, Qatar kwa ajili ya mazishi leo.
Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza siku tatu za maombolezo nchini kote kufuatia kuuawa shahidi Haniyah.