Taarifa ya IRGC inaeleza kuwa, jinai hiyo ya kigaidi iliyopelekea kuuawa shahidi Ismail Haniya ilipangwa na kutekelezwa na utawala haramu wa Israel kwa himaya na uungaji mkono wa serikali inayotenda jinai ya Marekani.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo inabainisha kuwa, shambulio lililopelekea kufa shahidi Ismail Haniya lilitekelezwa kwa kombora la masafa mafupi lililovikwa mada kali za milipuko yenye uzito wa karibu kilo saba. Shambulio hilo lilitekelezwa umbali wa masafa machache kutoka nje ya eneo la jengo alilokuwamo shahidi Ismail Haniya.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesisitiza katika taarifa hiyo kwamba, ulipizaji kisasi wa damu ya shahidi Ismail Haniya ni jambo lisilo na shaka, na utawala wenye chokochoko na wa kigaidi wa Kizayuni wa Israel utapata jibu la jinai hii ambalo ni "adhabu kali" kwa wakati na mahali mwafaka.
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, Ismail Haniya, ambaye alikuwa Tehran kuhudhuria hafla ya kuapishwa Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian, aliuawa pamoja na mlinzi wake katika shambulio la Israel kwenye jengo alilokuwa amefikia.
4229872