IQNA

Muqawama

Mjue Shahidi Ismail Haniya, Kutoka Ghaza hadi Tehran

12:04 - August 02, 2024
Habari ID: 3479212
IQNA-Shahidi Ismail Haniya Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) alikuwa mwanamapambano ambaye alijitolea maisha yake yote katika kuendesha mapambano dhidi ya maadui wa Uislamu.

Ismail Haniya alikuwa mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ambaye Mei 6 mwaka 2017 alishika wadhifa wa Mkuu Mpya wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas akichukua nafasi ya mtangulizi wake Khalid Mash'aal.  

Ismail Abdulsalam Ahmad Haniya maarufu kwa lakabu ya Abu Abdusalam alizaliwa tarehe January 29, 1962 katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina ya al Shati. Familia yake ilihamishwa kwa nguvu katika kijiji cha "Jurah" huko Ashkelon, katika maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu ya Palestina mnamo mwaka 1948. Alitunukiwa shahada ya udaktari wa heshima katika Chuo Kikuu cha Kiislamu katika Jiji la Gaza mwaka 2009;  alioa na kujaaliwa watoto 13. 

Elimu na kuanza harakati

Haniya alifuzu elimu yake ya msingi na sekondari katika shule za UNRWA na alitunukiwa diploma yake kutoka Kituo cha Al-Azhar; na kisha mwaka 1981 alianza masomo katika Chuo Kikuu cha Kiislamu katika mji wa Gaza ambapo alihitimu katika masomo ya fasihi ya lugha ya Kiarabu. 

Ismail Haniya alikuwa na kazi na majukumu mengine mengi katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Gaza kabla ya kuwa mjumbe wa kamati ya uongozi wa chuo hicho mwaka 1997. Alikuwa Mkuu wa Ofisi ya Sheikh Ahmad Yassin baada ya kuachiwa huru Sheikh Yassin. 

Haniyeh pia alikuwa mjumbe wa Kamati ya Ngazi ya Juu ya Majadiliano na Mwakilishi wa Hamas katika kamati kuu ya kufuatilia masuala ya makundi ya kitaifa na Kiislamu wakati wa Intifadha ya Pili. 

Utawala wa Kizayuni kwa mara ya kwanza mwaka 1987 na baada ya kupamba moto vuguvugu la Intifadha ya Kwanza ya Palestina ulimtia nguvuni Haniyeh na kumshikilia kwa siku18. 

Mwaka 1988 Ismail Haniya alikamatwa na kufungwa jela kwa mara ya pili kwa muda wa miezi sita. Mwaka 1989 pia Haniya alitiwa nguvuni akituhumiwa kuwa mwanachama wa Hamas na kisha kufungwa jela ambako alisalia huko kwa miaka mitatu. Kisha Haniya pamoja na viongozi wemgine 415 wa Palestina khususan viongozi wa harakati za Hamas na Jihadul Islami walibaidishwa katika eneo la Marj al-Zhour huko Lebabon na baadaye alirejea Gaza baada ya mwaka mmoja. 

Kunusurika mauaji

Tarehe 6 Septemba 2003 Ismail Haniyeh alinusurika kuuawa katika oparesheni ya kigaidi ambapo utawala wa Kizayuni ulikusudia kumuuwa kiongozi huyo wa Hamas pamoja na Sheikh Ahmad Yassin. 

Kisha aliingia bungeni kama Mkuu wa Orodha ya "Mabadiliko na Mageuzi" yenye mfungamano na harakati ya Hamas, ambayo ilishinda viti vingi katika uchaguzi wa bunge wa Januari 2006, na alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Palestina mwezi Februari 2006.

Hii ni katika hali ambayo tarehe 20 Oktoba 2006 Haniyeh na timu yake aliyokuwa amefuatana nayo walifyatuliwa risasi wakati wa machafuko huko Ukanda wa Gaza na mtu mmoja aliuliwa shahidi miongoni mwao.

Ndege za kivita za utawala wa Kizayuni  zilishambulia pia nyumba ya Haniyeh katika kambi ya al Shati katika vita vya siku 51 msimu wa kiangazi mwaka 2014.

Kuuawa shahidi Tehran

Hatimaye Ismail Haniyah Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas)  ameuawa shahidi leo alfajiri Jumatano Julai 31, baada ya kushambuliwa makazi yake hapa mjini Tehran. Alikuwa amefika jijini Tehran kuhudhuria hafla ya kuapishwa rais mpya wa Iran Masoud Pezeshkian. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbe maalumu baada ya kuuawa shahidi Ismail Haniya Mkuu wa Tawi la Kisiasa la HAMAS akisisitiza kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umejiandalia uwanja wa kuadhibiwa vikali.

Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Ayyatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo Jumatano ametoa ujumbe akisisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni ambao ni mtenda jinai na ni utawala wa kigaidi, umemuua shahidi mgeni wetu kipenzi kwenye nyumba yetu na kututia majonzi makubwa, hivyo utawala huo umejiandalia mazingira ya kuadhibiwa vikali.

Katika ujumbe wake huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, shahid Ismail Haniya ametumia miaka mingi ya umri wake kuendesha mapambano ya kishujaa na kujitolea muhanga roho yake katika njia ya haki na muda wote alikuwa tayari kwa ajili ya kufa shahidi katika mapambano hayo. Ametoa muhanga pia wanawe na watu wake wa karibu katika njia hiyo. Haniyeh amekufa shahidi katika njia ya Allah na kwa ajili ya kuwaokoa waja wa Mwenyezi Mungu. Lakini sisi kuhusu tukio hilo chungu na zito ambalo limefanyika ndani ya mipaka ya Jamhhuri ya Kiislamu, tunasema kwamba kulipiza kisasi damu yake ni jukumu na wajibu wetu. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran naye amesisitiza kuwa, Iran itawafanya wavamizi wa magaidi kujutia kitendo chao hicho cha uoga.

Huku akilaani mauaji ya Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, Masoud Pezeshkian, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X (zamani wa Twitter): Mshikamano kati ya mataifa mawili yenye fahari ya Iran na Palestina utakuwa na nguvu zaidi kuliko hapo awali, na njia ya muqawama na kutetea wanaokandamizwa itakuwa na nguvu zaidi kuliko hapo awali.

4229620

 

 

 

 

 

Habari zinazohusiana
captcha