Hajj Hussein Hamdan, mtaalamu na msomaji wa Qur'ani ambaye amehudumu katika majopo ya majaji katika mashindano mengi ya kimataifa ya Qur'ani, amezungumza na Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) na kusema kwamba pamoja na Jihadi na kufuatilia masuala yanayohusu Umma wa Kiislamu, kusoma aya za Qur'ani Tukufu ilikuwa miongoni mwa vipaumbele vya shahidi Nasrallah.
Kila alipokuwa akiitumikia Qur'ani Tukufu, Nasrallah alijihisi yuko karibu na Mungu, Hamdan alisema.
Ameongeza kuwa Nasrallah ni mfano wa watu wanaomcha Mwenyezi Mungu walioelezwa katika Khutba ya 193 ya Nahj al-Balagha, “Wakati wa usiku wanasimama kwa miguu wakisoma sehemu za Qur’ani na kuisoma kwa kipimo cha kutosha, wakiwa na huzuni katika nafsi zao na kutafuta kwayo dawa ya maradhi yao. Wakikutana na Aya inayoleta hamu (ya Pepo) wanaisoma kwa shauku, na roho zao huielekea kwa shauku, na wanaona kana kwamba iko mbele yao. Na wanapokutana na Aya iliyo na khofu (ya Jahannam) hutega masikio ya nyoyo zao kwa hiyo, na wanahisi kana kwamba sauti ya Jahannamu na vilio vyake vinafika masikioni mwao. Wanainama migongo yao na kusujudu juu ya vipaji vya nyuso zao, viganja vyao, magoti yao na vidole vyao vya miguu, na wanamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awaokoe.”
Ameongeza kuwa, Nasrallah alinufaika na mafundisho ya Qur'ani katika kukabiliana na madola ya kiburi na alikuwa mtu wa Jihadi kupitia utamaduni na mafundisho ya Qur'ani.
Hamdan ameongeza kuwa, Nasrallah alipenda sana kuandaa mashindano ya Qur'ani miongoni mwa nchi za mhimili wa muqawama kama vile mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Qari huyo mashuhuri amesisitiza zaidi kuwa, njia ya muqawama wa Lebanon ambayo ni ya makabiliano na utawala wa Kizayuni, kuilinda Lebanon na kuwasaidia wananchi wa Palestina hususan Ukanda wa Ghaza itaendelea baada ya kuuawa shahidi Nasrallah.
Sayyid Hassan Nasrallah aliuawa shahidi katika shambulizi kubwa la kigaidi la anga ambalo Israel ilitekeleza kusini mwa Beirut mnamo Septemba 27 kwa kutumia mabomu ya kivita yaliyotolewa na Marekani.
4239977