Meja Jenerali Mohammad Bagheri amesema kuwa, kwa operesheni yake ya kishujaa na ya kijasiri, Jeshi la Wanaanga la IRGC lililipiza kisasi kwa jinai nyingi za utawala wa Kizayuni.
Meja Jenerali Bagheri ameeleza kuwa oparesheni hiyo haikuvilenga vituo vya kiuchumi na viwanda vya utawala wa Kizayuni wala raia wa kawaida katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu (Israel); katika hali ambayo hilo lingewezekana kikamilifu.
Amesema, Jeshi la IRGC na vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran viko tayari iwe ni katika uga wa kiulinzi au kushambulia na kuwa vipo tayari kukariri mashambulizi yao tena kwa mara kadhaa.
Jenerali huyo mkuu amesema ingawa Iran ilikuwa na uwezo wa kugonga miundombinu ya kiuchumi na kiviwanda ya utawala wa Israel, ilijizuia kufanya hivyo.
Halikadalika amesema iwapo utawala wa Kizayuni ambao umefikia kiwango cha uwendawazimu hautadhibitiwa na Marekani na nchi za Ulaya na kutaka kuendeleza jinai zake au kuchukua hatua za kukiuka mamlaka ya kujitawala ya Iran, basi Iran itatekeleza tena kwa nguvu zaidi oparesheni kama ya Jumanne usiku na kushambulia miundo mbinu yote ya utawala huo. Meja Jenerali Bagheri amesema anataraji kuwa Marekani itaachana na mbinu yake ya zamani na kuushinikiza utawala wa Kizayuni ili eneo hili lipate amani.
3490109