Mahdawi aliachiliwa kutoka kizuizi cha uhamiaji baada ya jaji wa shirikisho huko Vermont kuamuru kuachiliwa kwake.
“Wiki mbili za kizuizini hadi sasa zimeonyesha madhara makubwa kwa mtu ambaye hajashitakiwa kwa kosa lolote,” alisema Geoffrey Crawford, jaji wa wilaya ya Marekani, katika kikao cha Jumatano. "Mahdawi, ninaamuru uachiliwe."
Katika uamuzi wake, Crawford alisema ushahidi uliopo mahakamani “unaashiria kuwa Mahdawi siyo mtu wa hatari ya kutoroka au tishio kwa jamii, na kuachiliwa kwake hakutavuruga mchakato wa kuondoshwa kwake nchini.”
Crawford aliagiza Mahdawi kuachiliwa kwa dhamana, akisubiri uamuzi wa kesi yake katika mahakama ya shirikisho.
Amri hiyo inamruhusu Mahdawi kuendelea kuishi Vermont na kusafiri hadi New York kuhudhuria masomo na kukutana na mawakili wake. Kesi yake katika mahakama ya shirikisho itaendelea sambamba na mashauri ya uhamiaji.
Crawford aliandika kuwa serikali “imeshindwa kuonyesha sababu yoyote halali ya kuendelea kumshikilia Bw. Mahdawi” na kwamba “kumuacha kizuizini kunaweza kuwa na athari ya kuzima uhuru wa kujieleza unaolindwa kikatiba.”
Mahdawi, mwenye 'Kadi ya Kijani' ya Marekani, alikuwa amekamatwa na kuamriwa kufukuzwa nchini na serikali ya Trump mnamo Aprili 14 wakati wa mahojiano ya uraia wake.
Mahdawi alikamatwa “kwa kulipiza kisasi moja kwa moja” kutokana na nafasi yake katika maandamano ya vyuo vikuu kupinga mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza.
Akiwa mkosoaji mashuhuri wa vita vya utawala wa Israel dhidi ya Gaza, Mahdawi alifanya mahojiano na kipindi cha 60 Minutes cha CBS Desemba iliyopita na kutoa mwanga kuhusu mauaji ya kimbari ya Israel katika eneo la Palestina.
Alizaliwa katika kambi ya wakimbizi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, na alihamia Marekani mwaka 2014 na kuanzisha Jumuiya ya Wanafunzi wa Kipalestina katika Chuo Kikuu cha Columbia.
Akiwa anakabiliwa na hatari ya kufukuzwa kwa nguvu, Mahdawi alijiunga na wanafunzi wengine kadhaa wanaoshikiliwa kwa kushiriki maandamano yanayounga mkono Palestina kwenye vyuo vikuu kote Marekani.
Rais wa Marekani Donald Trump ameanza kutekeleza kitisho cha kuwafukuza wanaharakati wasio raia wa Marekani wenye uhusiano na maandamano ya kuunga mkono Palestina, ambayo yalitikisa Marekani msimu uliopita wa kuchipua, huku wanafunzi wakifanya maandamano ya kila siku kwenye vyuo vikuu kote nchini kwa wiki kadhaa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, ambaye binafsi alitia saini amri ya kukamatwa kwake, alisema hivi karibuni kwamba Washington imefuta angalau visa za wanafunzi wa kigeni 300.
Maafisa wa Trump wamewatuhumu wanafunzi hao kwa kuwa “wenye kupingana na sera za kigeni na maslahi ya usalama wa taifa” ya Marekani kutokana na kulaani kwao vita vya miezi kadhaa vya mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza ulioko chini ya mzingiro.
3492897