IQNA

Maktaba ya Kitaifa ya Misri inahifadhi hati adimu za Qur’ani kutoka historia ya Kiislamu

23:49 - May 06, 2025
Habari ID: 3480647
IQNA-Maktaba na Makavazi ya Kitaifa ya Misri, inayojulikana kama Dar Al-Kutub, inahifadhi mkusanyiko wa kipekee wa hati za Qur’ani za kale na za kihistoria, baadhi yake zikiwa na zaidi ya miaka elfu moja.

Osama Talaat, mkuu wa Mamlaka ya Jumla ya Maktaba na Nyaraka za Kitaifa na profesa wa turathi za Kiislamu na Koptiki, alizungumza kuhusu hazina hiyo katika mahojiano ya televisheni na kituo cha ON TV cha Misri.

“Maktaba na Makavazi ya Kitaifa ni mojawapo ya taasisi muhimu zaidi za kitamaduni nchini Misri. Mwanzo wake unarejea katika karne ya 19,” alisema Talaat, akibainisha kuwa makavazi hiyo ilianzishwa mwaka 1828.

Kulingana na Talaat, nakala adimu za Qur’ani zilipewa misikiti maarufu, ikiwa ni pamoja na Msikiti wa kihistoria wa Amr ibn al-As mjini Cairo—uliokuwa msikiti wa taifa wa Misri wakati huo. Baadaye hati hizo zilihamishiwa kwenye Maktaba ya Kitaifa kwa ajili ya kuhifadhiwa.

“Maktaba ina  nakala za  Qur’ani za kipekee kutoka nyakati tofauti za kihistoria. Zinajulikana kwa uzuri wa sanaa na maandiko yake,” alisema.

Miongoni mwa nyaraka muhimu zaidi ni maandiko yanayojulikana kama Mushaf wa Uthman, yaliyoandikwa kwenye ngozi ya paa kwa maandishi ya mapema ya Kufi. “Hati hii haina alama za vokali wala nukta za diacritical, jambo ambalo lilikuwa la kawaida wakati huo. Waarabu waliweza kuisoma kwa uelewa wa asili,” alieleza Talaat.

Talaat pia alitaja nakala ya Qur’ani ya miaka 1,300 inayoaminika kuwa ya Imam Ja‘far al-Sadiq (AS), inayokadiriwa kuwa imeandikwa mwaka 148 AH (takriban 765 CE), na inaaminika na baadhi ya watu kuwa iliandikwa kwa mkono wake mwenyewe.

Hati nyingine adimu ni “Qur’ani ya Ibn Qalawun,” inayorejea enzi za Wamamluki na utawala wa familia ya Qalawun nchini Misri. Talaat aliielezea kuwa ni “moja ya nakala muhimu zaidi zinazoifadhiwa katika maktaba.”

Moja ya nyaraka maarufu ni “Qur’ani ya Qulijito,” zawadi kutoka kwa sultani wa Wamongolia nchini Iran kwa Sultan al-Nasir Muhammad ibn Qalawun wa Misri. “Hati hii imeorodheshwa katika Kumbukumbu ya Dunia ya UNESCO tangu 1992, chini ya mkusanyo wa Qur’ani za Wamamluki,” alisema.

Talaat alihitimisha kwa kusisitiza juu ya uhifadhi wa Qur’ani ya Qulijito, inayorejea mwaka 725 AH (takriban 1325 CE). “Imehifadhiwa katika hali yake ya awali, bila mabadiliko yoyote katika rangi au maandiko yake. Inabaki jinsi ilivyokuwa wakati wa utawala wa Sultan al-Nasir Muhammad.”

3492957

captcha