Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni iliyochapishwa na Al Jazeera, hati za Kiarabu, Kituruki na Kiajemi katika bara Ulaya, sawa na sanaa na fasihi ya Kiislamu, zilifika katika nchi zinazozungumza Kijerumani kuanzia Enzi za Kati kupitia uhusiano wa kidiplomasia, kibiashara na kijeshi.
Baadhi ya hati hizo zilikuwa zawadi za kifahari kwa wafalme na wakuu wa kifalme, huku nyingine zikiwa ni nyara za vita. Hati na kazi za sanaa ya Kiislamu zilizofika Ulaya mara nyingi zilimilikiwa na wakuu wa kifalme au hazina za makanisa. Mkusanyiko wa hati za Kiislamu na Mashariki mwa Dunia uliundwa barani Ulaya kupitia ukaribu wa kidiplomasia na Dola ya Kiosmani kuanzia karne ya 17 hadi ya 19. Hata hivyo, kutokana na mageuzi ya kisiasa na msukumo wa kisekula uliopunguza mamlaka ya makanisa, mikusanyiko hii ilibaki kutawanyika na bila mpangilio.
Uchunguzi wa kina kuhusu mazingira ambayo hati hizi 40,000 za Kiarabu zilipatikana katika maktaba kuu tatu za Ujerumani umeangazia uhusiano tata na unaobadilika kati ya Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini. Kituo cha Utafiti wa Tamaduni za Hati (Center for the Study of Manuscript Cultures) nchini Ujerumani, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Hamburg, kimechapisha tafiti kuhusu asili ya hati za Kiarabu na jinsi zilivyoingia katika maktaba za Kijerumani.
Maktaba za serikali za Berlin, Bavaria, na Maktaba ya Utafiti ya Gotha ndizo zinazohifadhi mikusanyiko mikubwa ya hati kutoka Mashariki. Profesa Tilman Seidensticker, mtaalamu wa masomo ya Kiislamu kutoka Idara ya Masomo ya Mashariki katika Chuo Kikuu cha Friedrich Schiller, Jena, anasema kuwa hati hizi zilifika katika maktaba kupitia usambazaji kutoka maktaba za zamani za Ujerumani Mashariki pamoja na kutoka katika nyumba za watawa na majumba ya kifalme ambako zilihifadhiwa katika miaka ya mwisho ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Wakati wa vita, mamlaka ya Ujerumani ilifuata sera ya kusambaza kazi za kitamaduni katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Kisovyeti, na idadi ndogo tu ya nakala za hati iliwekwa katika maktaba za Berlin na Gotha. Hati za Mashariki zilizoko katika Maktaba ya Gotha ni mfano bora wa namna ambavyo uhamishaji wa hati kwenda Umoja wa Kisovyeti haukumanisha upotevu wao. Mkusanyiko mzima wa zaidi ya hati 3,000 ulipelekwa Umoja wa Kisovyeti mwaka 1946 na kurudishwa salama mwaka 1956, miaka mitatu baada ya kifo cha Stalin.
Kwa mujibu wa Seidensticker, tafiti zilizochapishwa na Chuo Kikuu cha Hamburg zinaonyesha kuwa vitabu na hati nyingi, pamoja na baadhi ya maonyesho, ziliibwa kutokana na madhara ya vita. Hati za Kiarabu sasa zimewekwa katika maeneo ya usalama wa juu ndani ya maktaba za Ujerumani, na wasomi wana matumaini kuwa hazitasafirishwa tena kutoka vyumba vya usomaji.
Hati za Kiarabu hazikutokana na chanzo kimoja tu. Wanahistoria wamebaini ongezeko kubwa la hati zilizopatikana kati ya mwaka 1852 na 1887. Bajeti ya kawaida ya maktaba haikutosha kupata mkusanyiko huu wa gharama kubwa, hivyo ilihitaji msaada wa kifalme kutoka kwa Mfalme wa Prussia.
Maktaba ya pili kubwa iko Bavaria, mjini Munich, na kwa sasa inahifadhi hati za Kiislamu zipatazo 4,200. Mkusanyiko huu ulianza na Johann Albrecht Widmanstetter, mtaalamu wa masuala ya Mashariki (1506–1557), aliyefanya kazi kama mwanadiplomasia na mtafiti katika jamii za Kiarabu, maarufu kwa kuchapisha mapema Qur’ani – nakala zake bado zipo katika maktaba za Ujerumani.
Maktaba hiyo pia ilikuwa na nyara za vita kati ya majeshi ya Ulaya na Dola ya Kiosmani. Baadaye, nakala 60 za hati zilipelekwa katika maktaba hiyo kama zawadi kutoka kwa madaktari wawili wa ukoo wa kifalme wa Misri wa Khedivi.
Kwa mujibu wa Seidensticker, maktaba hiyo ilipokea pia vitabu vya thamani kutoka kwa mwanaorientalisti wa Kifaransa Étienne Marc Quatremère na hati 157 kutoka Yemen.
Idadi ya hati za Kiislamu na Mashariki iliongezeka kwa kasi katika nusu ya pili ya karne ya 20, kutokana na juhudi za maktaba ya Munich, ambapo mmoja wa maktaba alikuwa na shauku ya pekee kuhusu hati za Qur’ani. Alifaulu kununua nakala nyingi muhimu kwa wakati ambao bei ya vitabu vya aina hii ilikuwa bado chini. Maktaba hiyo sasa ina nakala 179 kamili au sehemu za Qur’ani Tukufu.
Katika mizozo kati ya Dola ya Kiosmani na mataifa ya Ulaya, maktaba za Ujerumani zilipata hati kwa njia zisizo za kawaida. Katika maktaba ya zamani ya Gotha, kuna hati 74 za Mashariki, baadhi zikiwa na maelezo yanayoonyesha kuwa zilikuwa nyara za vita. Hati hizo zina dondoo kutoka Qur’ani na Sunna.
Hati nyingi zilizoko katika maktaba za Ulaya ni ushahidi wa matukio maarufu ya kijeshi kama vile kuzingirwa kwa Vienna. Mnamo mwaka 1535, baada ya Mfalme Charles V kuizingira Tunis, maktaba na misikiti ya jiji hilo yaliporwa na Misahafu au nakala za Qur’ani zilipelekwa Heidelberg, na baadaye hadi Vatican.
Baada ya vita vya Lepanto mwaka 1571, kati ya Ulaya na Waturuki, hati 20 za Kiarabu, Kiajemi na Kituruki ziliangukia mikononi mwa Wazungu na kupelekwa katika Maktaba ya Escorial huko Madrid.
Waharamia wa Kihispania waliandika habari za usafirishaji wa hati kutoka Uarabuni hadi Ulaya. Mwaka 1611, waliteka mashua iliyokuwa karibu na pwani ya Magharibi mwa Morocco iliyobeba maktaba nzima ya Sultan Zaydan, iliyo kuwa na Makala ay nyaraka 3,000 hadi 4,000. Hati hizo ziliwasilishwa kwa Mfalme Philip III na kuwekwa katika Maktaba ya Kifalme ya Jumba la Watawa la San Lorenzo huko Escorial.
Hivyo basi, katika hatua za awali za uhamishaji wa hati za Kiarabu kwenda maktaba za Ujerumani, kabla ya vita na uporaji kuwa chanzo kikuu, maslahi ya kikoloni na kiuchumi yalichangia pakubwa. Wanahistoria wamebaini mashindano kati ya maktaba na makumbusho ya Ulaya katika kuunda mikusanyiko mikubwa ya hati zinazowakilisha utamaduni wa juu wa wakati huo.
3492662