IQNA

Idul al-Adha: Kumbukumbu ya Utiifu na Kujitolea kwa Mwenyezi Mungu

16:07 - June 06, 2025
Habari ID: 3480796
IQNA – Idul al-Adha ni miongoni mwa sikukuu tukufu zaidi katika kalenda ya Kiislamu, yenye mizizi katika tukio la kiroho lenye uzito mkubwa lililotajwa ndani ya Qur’ani Tukufu.

Sikukuu hii huadhimishwa kila mwaka tarehe 10 ya mwezi wa Dhul Hijjah, mwezi wa mwisho katika kalenda ya Kiislamu ya Hijria,  ikiwa ni kumbukumbu ya utiifu na unyenyekevu wa Mtume Ibrahim (amani iwe juu yake) na mwanawe Ismail (amani iwe juu yake), walipoitikia amri ya Mwenyezi Mungu kwa moyo wa imani na kujisalimisha.

Kwa mujibu wa mapokezi ya Kiislamu, Mwenyezi Mungu alimwamrisha Ibrahim amtoe mwanawe Ismail dhabihu, mtoto aliyemruzuku uzeeni. Bila kusita, baba na mwana walijiandaa kutekeleza amri ya Mola wao kwa moyo wa subira na yakini.

Hata hivyo, wakati Ibrahim alipokuwa karibu kutekeleza agizo hilo, Mwenyezi Mungu alimtuma Malaika Jibril (amani juu yake) na akamletea kondoo wa kuchinjwa badala ya Ismail. Tukio hili limeelezewa kwa uzito mkubwa katika Qur’ani, katika Surah As-Saaffat, aya 106 hadi 109:

“Hakika huu ulikuwa ni mtihani wa dhahiri. Basi tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu. Nasi tukamuachia (sifa njema) kwa waliokuja baadaye. Amani iwe juu ya Ibrahim.”

Tukio hili limefasiriwa na wanazuoni wengi wa Kiislamu kuwa ni mtihani wa kweli wa imani, Ikhlas (unyofu wa nia), na kujisalimisha kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Lengo kuu halikuwa tu kutoa dhabihu ya mwana, bali kuonyesha kiwango cha juu cha utiifu na kujitoa kwa ajili ya Mola.

Baadhi ya tafsiri pia zimeeleza kuwa tukio hili lilikuwa ni mabadiliko ya kihistoria kutoka desturi ya kale ya kutoa sadaka ya binadamu, ambayo ilikuwa ikifanywa na baadhi ya jamii za zamani, hadi kwenye mafundisho ya kiroho yenye misingi ya maadili na huruma.

Ujumbe mkuu unaopatikana katika tukio hili ni usafishaji wa moyo dhidi ya mapenzi ya dunia, na kuelekeza matendo yote kwa ajili ya radhi ya Mwenyezi Mungu peke yake.

Katika zama za sasa, ujumbe huu unaendelezwa na kuadhimishwa kwa namna ya kiishara wakati wa ibada ya Hija, ambapo Mahujaji huchinja mnyama halali wa miguu minne kama sehemu ya ibada hiyo tukufu.

Mbali na Mahujaji walio Makkah, Waislamu kote duniani pia hushiriki katika ibada hii ya kuchinja. Wanazuoni wengine wa Kiislamu wameieleza kuwa ni Wajib (lazima) kwa mwenye uwezo, ilhali wengine huiona kuwa ni Mustahab (inayopendelewa).

Ni kawaida pia kwa Waislamu kula sehemu ya nyama ya mnyama aliyechinjwa baada ya swala ya Idi kama sehemu ya furaha, shukrani, na kuenzi mafundisho ya Mtume Ibrahim na mwanawe , mithali ya watu wa ikhlasi na tawakkul.

3493339

captcha