IQNA

Maelfu ya Waislamu wamesherehekea Eid Katika Msikiti wa Kati wa Glasgow

16:51 - June 08, 2025
Habari ID: 3480805
IQNA – Maelfu ya waumini walikusanyika katika Msikiti wa Kati huko Glasgow, Scotland, kwa sala maalum kuadhimisha Idul Adha.

Maelfu ya Waislamu wamesherehekea Eid Katika Msikiti wa Kati wa GlasgowOmar Afzal kutoka Baraza la Waislamu wa Scotland amesema kwenye STV News: “Ni tarehe muhimu sana katika kalenda ya Kiislamu.

Nje ya msikiti, waumini walijumuika na familia na marafiki, wengi wao wakiwa wamevalia mavazi ya jadi kutoka mataifa kama Libya na Nigeria. 

Wakati huo huo, katika Bridgeton, jamii ya Waislamu wa Sudan ilikusanyika katika msikiti wa muda. 

Sudan imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu Aprili 15, 2023, baada ya mvutano kati ya jeshi na Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) kugeuka kuwa mapigano makubwa mjini Khartoum na sehemu zingine. 

Mahomed Arkou alisema: “Vita vimenidhuru kwa sababu sasa kwa zaidi ya Idi 25, nasherehekea nje ya Sudan.” 

“Siwezi kurudi nyumbani kwa sababu ya ukosefu wa usalama, kwa sababu ya vita. Hali ni ngumu sana.” 

Kujumuika kula pamoja ni sehemu kuu ya sherehe za Idi, ambapo familia na marafiki hukutana kuswali na kisha kula pamoja kwa moyo wa ukarimu na imani. Huko Glasgow, kikundi kidogo kutoka jamii ya Wabangladeshi kilikusanyika katika nyumba binafsi kusherehekea idi. 

Shari Ali alisema: “Ni wakati ambapo sisi sote tunakusanyika kama familia. Hata ikiwa hatuhusiani kwa damu, ni watu tuliowajua kwa muda mrefu katika maisha yetu yenye shughuli nyingi, na hatupatani mara kwa mara.” 

“Wakati wa Idi, kula pamoja ni fursa ya kufahamiana kwa karibu zaidi.” 

Idul al-Adha ni miongoni mwa sikukuu tukufu zaidi katika kalenda ya Kiislamu, yenye mizizi katika tukio la kiroho lenye uzito mkubwa lililotajwa ndani ya Qur’ani Tukufu.

Sikukuu hii huadhimishwa kila mwaka tarehe 10 ya mwezi wa Dhul Hijjah, mwezi wa mwisho katika kalenda ya Kiislamu ya Hijria,  ikiwa ni kumbukumbu ya utiifu na unyenyekevu wa Mtume Ibrahim (amani iwe juu yake) na mwanawe Ismail (amani iwe juu yake), walipoitikia amri ya Mwenyezi Mungu kwa moyo wa imani na kujisalimisha.

Kwa mujibu wa mapokezi ya Kiislamu, Mwenyezi Mungu alimwamrisha Ibrahim amtoe mwanawe Ismail dhabihu, mtoto aliyemruzuku uzeeni. Bila kusita, baba na mwana walijiandaa kutekeleza amri ya Mola wao kwa moyo wa subira na yakini.

Hata hivyo, wakati Ibrahim alipokuwa karibu kutekeleza agizo hilo, Mwenyezi Mungu alimtuma Malaika Jibril (amani juu yake) na akamletea kondoo wa kuchinjwa badala ya Ismail. Tukio hili limeelezewa kwa uzito mkubwa katika Qur’ani, katika Surah As-Saaffat, aya 106 hadi 109:

“Hakika huu ulikuwa ni mtihani wa dhahiri. Basi tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu. Nasi tukamuachia (sifa njema) kwa waliokuja baadaye. Amani iwe juu ya Ibrahim.”

3493359

captcha