IQNA

Khatibu wa Sala ya Idi Tehran: Idul Adha ni Sikukuu ya Umoja, Ibada na Kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu

16:19 - June 06, 2025
Habari ID: 3480797
IQNA – Akiwatakia heri ya Idul Adha Waislamu kote duniani, Khatibu wa Swala ya Idi iliyosaliwa leo Tehran ameielezea Idihii tukufu kuwa ni sikukuu ya umoja wa Ummah wa Kiislamu, na maadhimisho ya ibada na kujisalimisha kwa Mola.

Hujjatul Islam Sayyid Mohammad Hassan Abutorabifard aliongoza Swala ya Idul Adha siku ya Ijumaa asubuhi katika Chuo Kikuu cha Tehran.

Katika khutba yake ya kwanza, alisema: "Leo ni Idul Adha, siku ambapo bendera ya ibada na kujitolea iliinuliwa juu katika kilele cha maisha kwa mikono thabiti ya mwanadamu bora kabisa aliyeishi,Nabii Ibrahim (Amani iwe juu yake). Manabii wote wa Mwenyezi Mungu walimfuata katika njia aliyoainisha. Bendera hiyo aliyoibeba kwa fahari, ilienezwa kwa heshima kote ulimwenguni."

Akiendelea kufafanua, alieleza kuwa Nabii Ibrahim (AS) ni mfano wa daraja na heshima ambayo Mwenyezi Mungu amemkusudia mwanadamu. Alimtaja Mtume huyo kuwa kielelezo cha akili, elimu, yakini, ujasiri, na msimamo thabiti katika njia ya haki, huku akipambana na shirki na ukafiri, na akionyesha moyo wa kujitolea kwa ajili ya radhi za Mwenyezi Mungu.

Katika khutba ya pili, Hujjatul Islam Abutorabifard aligusia pia maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Imam Ruhullah Khomeini (Rahmatullahi Alayh) yaliyofanyika mapema wiki hii. Alisisitiza nafasi ya kihistoria ya Imam huyo katika kuleta mwamko wa Kiislamu na kuhuisha thamani za Qur’ani katika jamii ya kisasa.

Imam Khomeini (MA) alifanikiwa kuleta mageuzi makubwa nchini Iran na kuufanya Umma wa Kiislamu kuwa nguvu mpya inayozidi kunawiri katika ulimwengu wa sasa.

Aidha, alimshukuru taifa la Iran kwa kushiriki kwa mamilioni katika kumbukumbu za miaka 36 tangu kufariki dunia kwa Imam Khomeini (MA), mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, pamoja na kusikiliza hotuba yenye busara ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei katika maadhimisho hayo.

Khatibu wa Swala ya Idul Adha iliyoswaliwa leo mjini Tehran pia aliwapongeza wananchi wa Kiislamu wa Iran, hususan vijana, kwa kushiriki kwa wingi katika Dua ya Siku ya Arafa. Alisisitiza kuwa taifa la Iran limepasi katika chuo cha Ahlul Bayt (AS). Vilevile, alieleza kuwa Ghaza na taifa la Palestina kwa ujumla limeonyesha Muqawama wa kihistoria, akisisitiza kuwa huo ni mfano wa nguvu ya subira yenye chimbuko lake kutoka kwa Nabii Ibrahim (AS).

"Taifa la Palestina limesimama imara kwa zaidi ya mwaka mmoja kupambana na ulimwengu wa kiburi. Pia limekabiliana na uungaji mkono wa kisiasa, kijeshi, silaha, na usimamizi wa Marekani kwa jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya Palestina," alisema.

3493343

 

captcha