Mashambulizi ya anga yalilenga Msikiti wa Al-Hassan katika kitongoji cha Al-Tuffah, mashariki mwa Jiji la Gaza, takriban saa 11 kasorobo asubuhi, Novemba 16, 2023. Ndege za Israel zilidondosha bomu moja au mbili bila onyo la awali, na kusababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 15 na kujeruhi wengine wengi.
Msikiti huo ambao ulikuwa mkubwa zaidi katika eneo hilo ulibomolewa ndani ya sekunde chache na kuua waumini wote waliokuwapo. Miili mingi ilikuwa vipande vipande, kulingana na shirika la kitiba la kutetea haki za binadamu la Euro-Med Human Rights Monitor.
"Hakuna ushahidi uliopatikana wa shabaha zozote za kijeshi, kama vile vitu au watu wenye silaha, ndani ya msikiti au katika eneo linalozunguka wakati wa shambulio hilo," mfuatiliaji alisema katika ripoti ya Alhamisi.
Mbali na vifo vilivyotokea ndani ya msikiti huo, nyumba na majengo ya jirani, zikiwemo gereji na maduka ya useremala, yalipata uharibifu mkubwa na kusababisha majeruhi zaidi wakiwemo wanawake, watoto na vikongwe. Watu walioshuhudia tukio hilo walisema lilikuwa na uharibifu mkubwa, huku miili mingi ikiwa haijatambulika kutokana na nguvu ya mlipuko huo.
Uchunguzi hadi sasa umethibitisha utambulisho wa wahasiriwa 10 waliouawa katika mlipuko huo, akiwemo msichana mdogo, mwanamke na wanaume wanane, wawili kati yao walikuwa wazee.
Katika kujibu taarifa yake, Euro-Med imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuzingatia wajibu wake wa kisheria kwa kuchukua hatua za haraka kusitisha mauaji ya kimbari yanayoendelea Gaza, ikisisitiza kuwa kuzuia na kuadhibu ukatili huo ni wajibu wa kisheria kwa mataifa yote.
Wizara ya afya ya Gaza imeripoti kuwa tangu Oktoba 7 hadi sasa utawala haramu wa Israel umeua takriban Wapalestina 45,129 na wengine 107,338 kujeruhiwa. Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imethibitisha kuwa takwimu hizo ni za kuaminika, ikibainisha kuwa wengi wa waliofariki ni wanawake na watoto.
3491119