Wakati jumuiya ya kimataifa ikiadhimisha Siku ya Watoto Duniani Jumanne, Novemba 20, gazeti la kila siku la Jordan la al-Ghadd lilichapisha ripoti kuhusu jinsi vita vya utawala wa Israel vimewaathiri watoto katika Ukanda wa Gaza.
Taarifa hiyo imesema takriban watoto na vijana wote wa Gaza wamepata madhara ya afya ya akili kutokana na vita hivyo, na wanasaikolojia na wanasosholojia wanaamini kwamba uharibifu wa kisaikolojia wa vita utaendelea kuwaathiri kwa muda mrefu.
Kujipata katikak halisi ya vita na ukatili unaofanywa na majeshi ya utawala wa Kizayuni, vifo vya wanafamilia, marafiki na majirani, ukosefu wa usalama, ukosefu wa upatikanaji wa mahitaji ya kimsingi na mambo mengine ya vita vinaweza kusababisha mfadhaiko na masuala mengine ya kisaikolojia miongoni mwa watu, hasa watoto na vijana.
Wataalamu wanasema hali hiyo inaweza kuathiri maisha yao na tabia zao kwa muda mrefu, na hivyo wametoa wito wa juhudi za kuwarudisha katika maisha ya kawaida kupitia programu maalum za kisaikolojia.
Hamoud Alimat, profesa wa sosholojia katika chuo kikuu cha Qatar, anasema vita huacha athari mbaya kwa watoto kiakili na kihisia na kuunda vibaya maadili na tabia zao.
Ameongeza kuwa watoto wa Gaza wanakabiliwa na msongo wa mawazo, wasiwasi, jinamizi, kukosa umakini na kutoweza kufanya shughuli za kila siku na kwamba hayo ni baadhi tu ya matatizo ambayo watoto hao wanakumbana nayo katika maisha yao ya kila siku.
Naye Nael al-Adwan, mwanasaikolojia, anasema kinachotokea katika vita, kama vile kifo, mabomu na uharibifu wa nyumba, shule na hospitali, huwaacha watoto chini ya shinikizo kubwa la kiakili na kisaikolojia na husababisha magonjwa ya akili kama vile wasiwasi.
Haya yangeathiri nyanja zote za maisha ya watoto kwa muda mrefu, anabainisha. Utawala wa Israel ulianzisha vita vyake vya mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba 2023.Hadi sasa zaidi ya Wapalestina 44,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto wameuawa katika hujuma hiyo ya kinyama.
Kwa mujibu wa maafisa wa Gaza, zaidi ya watoto 17,000 ni miongoni mwa mashahidi, huku karibu watoto 43,000 wamepoteza mzazi mmoja au wote wawili. Aidha, watoto 3,500 katika eneo la pwani wako katika hatari ya kufariki kutokana na utapiamlo. Na kuhusu elimu, wavulana na wasichana wapatao 620,000 huko Gaza hawako shuleni kwa sababu ya vita.
3490756