Safaa Ali Hussein, afisa wa idara hiyo, alisema: "Idara yetu imeandaa mpango mpana wa kuhakikisha mazingira yanafaa na yenye afya kwa wafanya ziara wakati wa Muharram kwa kuweka mifumo ya hali ya juu ya kupoeza katika eneo lote la Haram."
Alifafanua kuwa mpango huo unahusisha uwekaji wa mifumo ya kupozea yenye uwezo wa jumla ya tani zaidi ya 9,000. Lengo kuu ni udhibiti wa hali ya hewa katika njia za kuingia na kutoka eneo hilo takatifu ili kuhudumia wimbi kubwa la wageni.
"Joto la kupozea ndani ya ukumbi limewekwa kubaki kati ya nyuzi joto 24 na 26," alibainisha, "ambayo husaidia kuzuia magonjwa yanayosababishwa na mabadiliko ya ghafla kati ya joto la ndani na nje."
Hussein pia aliangazia uzinduzi wa mfumo mpya ulioundwa kudhibiti shinikizo chanya na hasi la hewa ndani ya kaburi hilo. "Mfumo huu una jukumu muhimu katika kutoa nje hewa iliyochafuliwa na kupunguza hatari za kupumua hewa hiyo," aliongeza, akisisitiza kwamba operesheni nzima inasimamiwa na kufuatiliwa na wataalamu wa Iraq.
Mamilioni ya wafanyaziara kutoka Iraq na nchi nyingine hutembelea maeneo matakatifu huko Karbala wakati wa mwezi wa maombolezo wa Muharram.
Waislamu wa madhehebu ya Shia, na wengine duniani kote, huadhimisha kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) kila mwaka wakati wa Muharram.
Imam wa tatu wa Shia (AS) na kundi la familia yake na masahaba waliuawa kishahidi huko Karbala mnamo tarehe 10 Muharram (Ashura), 61 Hijria sawa na 680 Miladia, na jeshi la Yazid bin Muawiya.
Mwaka huu Ashura itaadhimishwa Jumapili Julai 6.
3493711