IQNA

Wahusika wa Karbala /3

Waliokosa muono wa mbali hawakufuatana na Imam Hussein kwenda Karbala

19:31 - September 14, 2022
Habari ID: 3475784
TEHRAN (IQNA) – Tukio la Karbala lina mafunzo mengi kwa wanadamu. Katika Vita vya Karbala vya mwaka 61 Hijria au 680 Miladia, mrengo wa haki na ukweli ulikabiliana na mrengo wa batili na uwongo.

Miaka 1383 iliyopita tarehe 10 Muharram katika siku ya Ashura, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala katika Iraq ya leo.

Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah. Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya.

Katika mapambano ya Karbala, sifa za wahusika zilibainika kulingana na chaguzi walizofanya.

Kulikuwa na baadhi ya watu ambao hawakuhudhuria vita hivyo na kushindwa kupigana bega kwa bega na Imam Hussein (AS). Baadhi yao walifanya hivyo kwa sababu walikosa muono wa mbali au utambuzi na walikuwa na shaka juu ya usahihi wa uamuzi ambao Imam (AS) alikuwa ameufanya.

Miongoni mwao tunaweza kuwataja  Muḥammad ibn al-Ḥanafīyya , Abdullah ibn Jafar, na Omar ibn Ali, ndugu wa kambo wa Imam Hussein(AS).

Badala ya kuandamana naye, Muḥammad ibn al-Ḥanafīyya  alimshauri Imam Hussein (AS) akimbilie Yemen. Alifikiri kwamba ingetosha kwa Imam (AS) kuokoa maisha yake. Alishindwa kutambua kwamba Imam Hussein (AS) alikuwa kwenye njia ambayo ilihitaji mapambano na kubainisha mikengeuko ya jamii. Alishindwa kutambua kwamba Imam Hussein (AS) hakuwa na woga wa kuuawa kishahidi.

Omar ibn Ali, kaka mwingine wa kambo wa Imam (AS), sio tu kwamba hakufuatana naye hadi Karbala bali pia alishindwa kuungana na Mukhtar. Badala yake, alionyesha uadui kwa Imam Sajjad (AS) na akajiunga na kambi ya ibn Zubair, ambaye alikuwa adui wa Mukhtar.

Suleiman ibn Sard Khazaei alikuwa Mwislamu mashuhuri wa Shia mwenye hadhi ya juu ya kijamii. Aliposikia habari za kifo cha Mu'awiyah na kurithiwa kwa Yazid na kujua kwamba Imam Hussein (AS) yuko Makka na alikuwa amekataa kutoa utii kwa Yazid, aliitisha mkutano huko Kufa kwa kushirikisha watu mashuhuri wa mji huo.

Aliwajulisha kuhusu hali hiyo na kukataa kwa Imam (AS) kutoa kiapo cha utii kwa Yazid, akiwataka kumwandikia barua Imam Hussein (AS) aje Kufa ili waweze kupigana mbele ya uwongo (Yazid).

Washiriki wote katika mkutano walikubaliana naye na kuandika barua. Ilikuwa ni barua ya kwanza kutoka kwa watu wa Kufa kwenda kwa Imam Hussein (AS) na Suleiman ndiye aliyekuwa wa kwanza kusaini.

Punde msururu wa barua kutoka Kufa kwenda kwa Imam Hussein (AS) ulikuja. Hata baadhi ya Waislamu wa Kisunni na pia baadhi ya wale wanaojulikana kuwaunga mkono Bani Ummayya waliandika barua.

Suleiman, hata hivyo, ambaye wakati fulani aliacha kumuunga mkono Imam Ali (AS), kwa mara nyingine tena alionyesha ukosefu wake wa utambuzi. Alikataa kwenda Karbala, akitaja amri ya kutotoka nje katika Kufa kama kisingizio.

captcha