Haram hiyo, moja ya maeneo matukufu kabisa kwa Waislamu wa Madhehebu ya Shia, imeeleza juhudi zake za hivi karibuni ili kuhudumia Wafanyaziyara wanaotarajiwa kufika kwa wingi katika tukio hili la kidini ambalo ni miongoni mwa mikusanyiko mikubwa zaidi ya kila mwaka duniani.
Osama Al-Baghdadi, mkurugenzi wa kamati ya Arbaeen katika haram hiyo, alisema kuwa hatua kadhaa zimechukuliwa mwaka huu ili kuboresha huduma kwa wageni. “Mbali na maeneo ambayo hutengwa kila mwaka kwa ajili ya malazi, viyoyozi, usafi, na huduma nyingine, maelfu ya mita za mraba zimeongezwa ili kupanua uwezo wetu,” alieleza.
Aliongeza kuwa maeneo haya mapya yatahusisha miavuli ya kivuli, mazulia, mifumo ya kupoza hewa, upatikanaji wa maji salama ya kunywa, usambazaji wa chakula, na huduma nyingine za lazima. “Tumeandaa pia ushiriki wa watumishi wa kujitolea waliopata mafunzo maalum nchini Iran, kama ilivyofanyika katika miaka iliyopita,” Al-Baghdadi aliongeza.
Akizungumzia kuhusu usajili wa kujitolea, alifafanua kuwa maombi ya moja kwa moja wakati wa Arbaeen hayapokelewi. “Pamoja na hamasa kubwa kutoka kwa waumini wanaotamani kuhudumia mahujaji, haram inaweza tu kupokea wale waliochaguliwa rasmi na waliopatiwa mafunzo mapema,” alisema.
Al-Baghdadi alisisitiza dhamira ya timu ya haram, akisema: “Wajibu wetu ni kuwatumikia Wafanyaziyara wa Ahlul Bayt (AS) kwa ikhlasi. Tunatarajia kuwa mwaka huu, kama miaka iliyopita, tutatoa huduma bora na kuhakikisha mahujaji wanakamilisha ziara yao Najaf kwa salama na amani.”
Kwa kuzingatia uwezo mdogo wa jiji la Najaf na idadi kubwa ya wageni wanaotarajiwa kuwasili, Al-Baghdadi aliwashauri Wafanyaziyara kuendelea na safari yao kuelekea Karbala mara tu baada ya kumaliza ibada zao Najaf.
“Tunawahimiza mahujaji wamalize ziara yao kwa fahamu na tafakuri ya kiroho, kisha waendelee kwa utulivu kuelekea Karbala. Hii itasaidia kupunguza msongamano na kurahisisha utoaji wa huduma bora kwa wale watakaowasili baadaye,” alieleza.
Arbaeen ni kumbukumbu ya siku ya arobaini tangu tukio la Ashura, ambalo ni siku ya kuuawa shahidi kwa mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), yaani Imam Hussein (AS).
Kila mwaka, maelfu ya Mashia kutoka pande mbalimbali za dunia hukusanyika Karbala, mahali alipozikwa Imam Hussein (AS), kwa ajili ya kufanya ibada na maombolezo.
Wafanyaziyara hao, wengi wao wakitokea Iraq na Iran, husafiri kwa miguu umbali mrefu kuelekea mji huo mtukufu. Iran pia hutuma msafara wa Qur’ani, ujulikanao kama Msafara wa Nuur, kuelekea Iraq wakati wa matembezi ya Arbaeen.
Wanachama wa Msafara wa Nuur kutoka Iran hufanya shughuli mbalimbali za Qur’ani na kidini, ikiwemo usomaji wa Qur’ani, Adhana (wito wa swala), na Tawasheeh (kaswida za Kiislamu), katika barabara kati ya Najaf na Karbala, pamoja na maeneo mengine katika msafara wa Arbaeen.
/3493976