"Matembezi ya Arbaeen yana jukumu kubwa katika kueneza maadili ya kidini," Hujjatul Islam Seyyed Kazem Seyyed-Bagheri, mwanachama wa kitivo katika Taasisi ya Utafiti ya Utamaduni na Mawazo ya Kiislamu, aliiambia IQNA.
“Ujumbe wa Imam Hussein (AS) ulikuwa ni kueneza uadilifu na uhuru na kubomoa miundo ya ukandamizaji na dhulma; kwa hivyo, matembezi ya Arbaeen yanapaswa kuakisi mapambano haya dhidi ya madhalimu wa zama hizi, hasa kwa vile tukio la mwaka huu linasadifiana na ukatili unaoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Waislamu huko Ghaza,” aliongeza.
"Arbaeen inapaswa kutumika kama mkusanyiko wa kimataifa kwa wapenda uhuru kuinua bendera ya haki na uhuru, kuhakikisha kwamba kila mtu anayeshiriki katika matembezi ya Arbaeen anahisi kuwezeshwa na ujumbe huu," alisisitiza.
Maadhimisho ya Arbaeen hufanyika siku ya 40 baada ya Ashura, ukumbusho adhimu wa kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) ambaye aliuawa shahdi na jeshi katili la la Yazid katika vita vya Karbala mwaka 61 Hijria sawa na 680 Miladia.
Kila mwaka mamilioni ya Mashia na pia idadi kubwa ya wasiokuwa Mashia humiminika katika mji Karbala nchini Iraq, mji ulipo Haram Tukufu ya Imam Hussein (AS) ili kushiriki katika shughuli za maombolezo. Wafanya ziara, hasa kutoka Iraq na Iran, husafiri mamia ya kilomita kwa miguu hadi mji mtakatifu wa Karbala. Arbaeen ya mwaka huu inatarajiwa kuanguka mnamo Agosti 25, kulingana na kuonekana kwa mwezi.
Harakati ya mapambano ya Imam Hussein (AS) dhidi ya dhulma na ufisadi wa utawala wa Bani Umayya ilijaa hamasa, kujitolea na kusabilia kila kitu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, haki na uadilifu, na kwa sababu hiyo imegusa sana nyoyo za Waislamu na hata wapenda haki na kweli wasio Waislamu. Harakati hiyo ya Imam Hussein (AS) inaendelea kuibua vuguvugu na hamasa ya aina yake ndani ya nafsi za wapenzi wa mtukufu huyo.
3489623