Kwa mujibu wa ripoti ya Al-Watan, Al-Baraa amekamilisha kuhifadhi Qur’ani yote licha ya milipuko isiyokoma Gaza, ngurumo za ndege za kivita, na amri ya kuhamishwa kutoka maeneo yao, hali ambayo imewanyang’anya watu wa Gaza amani na utulivu.
Mtoto huyu wa miaka 12 alijawa na furaha na fahari alipofanikiwa kukamilisha kuhifadhi Qur’ani, licha ya maangamizi, mauaji ya kimbari, na vita vinavyoendelea dhidi ya watu wa Gaza.
Baba yake Al-Baraa aliuawa shahidi mwaka jana, na tangu wakati huo amekuwa akihamishwa mara kadhaa, akiishi katika mazingira yanayokosa hata mahitaji ya msingi ya kibinadamu.
Kwa mujibu wa mjomba wake kupitia akaunti rasmi ya Instagram, Al-Baraa pia alipoteza binamu yake Ahmad, aliyekuwa rika lake na aliyekuwa mshindani wake katika kuhifadhi Qur’ani.
Kama alivyoahidi baba yake kabla ya kuuliwa shahidi, Al-Baraa alijitahidi na kufanikisha kuhifadhi Qur’ani Tukufu yote.
Aliwasomea aya za mwisho za Surah Al-Baqarah kwa shangazi yake Noor Al-Huda, ambaye alipoteza watoto wake mwaka uliopita. Kisha akaanza kusoma Surah Al-Fatihah kwa mama yake, Hibatullah, ambaye machozi ya furaha na fahari yalimtoka kwa mafanikio ya mwanawe.
Video ya Al-Baraa baada ya kukamilisha kuhifadhi Qur’ani yote ilisambazwa mitandaoni, na ikapokelewa kwa hisia kali, huku watumiaji wa mitandao wakitoa maoni yao ya kuunga mkono.
Mtumiaji mmoja aliandika: “Mwenyezi Mungu amlete kheri na manufaa kwa Umma wa Kiislamu kupitia mhifadhi huyu wa Qur’ani, na amfanye kuwa nuru ya macho ya mama yake na mbeba bora wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu.”
Mwingine aliandika: “Enyi watu wa Gaza, jinsi mlivyo safi! Ninyi ni kielelezo cha taifa. Mwenyezi Mungu akubariki na akulinde, ewe Al-Baraa.”
3494585