Nchini Yemen maandamano makubwa yamefanyika katika mikoa wa Saada ambapo wananchi wametoa nara za kulaani hujuma ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na pia jinai ya mauaji ya kimbari ya utawala huo dhidi ya Gaza.
Katika miji ya Baghdad, Karbala, na Kufa nchini Iraq, maelfu wamejitokeza mitaani kuutaja utawala haramu wa Israel na Marekani kuwa maadu wakuu wa mataifa ya Waislamu.
Wamesema utawala wa Kizayuni wa Israel umekiuka maadili yote ya kibinadamu kwa kushambulia mahospitali, vituo vya kielimu na maeneo mengine ya raia nchini Iran. Waandamanaji waliokuwa na hasira pia wameteketeza moto bendera za utawala haramu wa Israel.
Maandamano sawa na hayo yamefanyika Pakistan katika miji ya Islamabad, Lahore na Karachi.
Huku wakiwa wanapeperusha bendera za Pakistan na Iran, waandamanaji walitoa nara dhidi ya Israel na Marekani sambamba na kutangaza kufungamana na operesheni za kijeshi za Iran dhidi ya Israel.
Nchini Lebanon pia kumefanyika maandamano katika mji mkuu, Beirut kulaani jinai za Israel dhidi ya Iran na Gaza.
Halikadhalika wanazuoni wa Kiislamu wa Lebanon na Palestina wamekutana huko Tyre, Lebanon na kulaani uchokozi wa Israel dhidi ya Iran. Aidha wamelaani vikali vitisho vya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.
Wazungumzaji katika kikao hicho wamesema Iran inakabiliana na ugaidi wa Marekani na utawala wa Kizayuni na kuongeza kuwa huu ni ugaidi usiotambua maadili ya ubinadamu, kinga ya vyombo vya habari na hukiuka kiholela sheria na kanuni za kimataifa. Wanazuoni hao wa Kiislamu wa Palestina na Lebanon wametoa wito kwa Waislamu duniani kote kusimama dhidi ya mradi wa Marekani na utawala wa Kizayuni ambao unaelnga kuangamiza Palestina, Lebanon, Iran, Syria, Iraq na Yemen.
3493516