IQNA

Mchango wa Wanawake Katika Maonyesho ya Kimataifa ya Qur’ani Tehran

14:16 - December 11, 2025
Habari ID: 3481645
IQNA – Afisa wa Wizara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu Iran amesisitiza nafasi muhimu ya wanawake katika Maonyesho ya Kimataifa ya Qur’ani ambayo hufanyika Tehran kila mwaka.

Hujjat-ul-Islam Hamidreza Arbab Soleimani, Naibu Waziri wa Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu na Mkuu wa Kituo cha Juu cha Qur’ani na Familia katika wizara hiyo, alikutana Jumatano na wanaharakati wa Qur’ani wanawake, sambamba na maadhimisho ya kuzaliwa kwa Bibi Fatima Zahra (SA), siku ambayo pia huadhimishwa kama Siku ya Mwanamke nchini Iran..

Katika hotuba yake, aliusifu mchango mkubwa wa wanawake katika Maonyesho ya Kimataifa ya Qur’ani, na akawahimiza wanaharakati hao kuwasilisha mapendekezo ya kuboresha programu za maonyesho hayo, pamoja na kutambulisha wanazuoni na wahusika wenye sifa ili meza ya kitamaduni ya mwezi mtukufu wa Ramadhani iwe na tija zaidi kuliko miaka iliyopita.

Maonyesho hayo ya Qur’ani hufanyika kila mwaka katika mwezi wa Ramadhani chini ya Wizara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu ya Iran, kwa lengo la kueneza mafundisho ya Qur’ani na kukuza shughuli za Qur’ani nchini. Huwasilisha mafanikio mapya ya Qur’ani pamoja na bidhaa mbalimbali zinazolenga kuikuza Kitabu Kitukufu.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Hujjat-ul-Islam Arbab Soleimani alitambua na kupongeza kazi za Zakiyeh Abdollahian, Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Qur’ani ya Wanawake, pamoja na wawakilishi wa taasisi na vituo vya Qur’ani waliohudhuria hafla hiyo. Aliwahimiza wanawake kutumia uwezo wao kikamilifu katika kueneza mafundisho ya Qur’ani na Ahlul-Bayt (AS).

Alisema: “Ripoti zinaonyesha kuwa katika baadhi ya maeneo, ikiwemo shughuli za watafiti wanawake, bado tunakabiliwa na changamoto zinazopaswa kushughulikiwa haraka. Ni muhimu kuunda kikosi kazi maalumu kwa ajili ya watafiti wa Qur’ani wanawake ili masuala kama vibali, changamoto za kitaasisi na mapendekezo yashughulikiwe kwa mpangilio.”

Akaongeza kuwa: “Kwa uzoefu wangu, nimejifunza kuwa kuzoea Qur’ani kila siku ni jambo la lazima, na kila mhusika wa shughuli za Qur’ani anapaswa kukamilisha kozi ya tafsiri.”

Mwanazuoni huyo alisisitiza kuwa jukumu kuu la Wizara ya Utamaduni ni kuimarisha utamaduni wa jamii na kunufaika na hazina za kimaanawi na kimada zilizomo ndani ya Qur’ani Tukufu. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuipa familia kipaumbele sambamba na shughuli za kijamii.

4322208

captcha