IQNA

Diplomasia ya Kiislamu

Rais wa Iran ahutubia kikao cha D8, ahimiza umoja kati ya Waislamu ili kukabiliana na uadui wa Israel

23:31 - December 19, 2024
Habari ID: 3479923
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesisitiza ulazima wa kuwepo umoja kati ya mataifa ya Kiislamu, na kutilia mkazo udharura wa kuchukuliwa hatua za pamoja ili kukabiliana na uchokozi wa utawala wa Israel.

Akihutubia katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za kundi la D8 huko Cairo, Misri mapema leo Alhamisi, Rais Pezeshkian amesema kuwa nchi za Kiislamu zinapasa kuwa na umoja na kusimama dhidi ya hujuma na chokochoko za utawala wa Kizayuni. 

"Ni wajibu wetu wa kidini, kisheria na kibinadamu kuchukua hatua za haraka na za kivitendo ili kuzuia madhara zaidi kwa wapendwa wetu katika maeneo yaliyokumbwa na migogoro”, amesisitiza Rais Pezeshkian.

Rais wa Iran pia amesema kuwa anatumai nchi wanachama wa D8 zitaimarisha uhusiano na kuchukua hatua za kustawisha ushirikiano katika kipindi hiki ambapo Misri ni mwenyekiti wa kundi hilo. 

Rais wa Iran amesisitiza zaidi kwamba mipango muhimu ya ujenzi wa maeneo yaliyoharibiwa na vita lazima isalie miongoni mwa matakwa ya juu ya D-8, pamoja na yale ya mashirika mengine ya kimataifa.

"Ningependa kusisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha na kuunga mkono makubaliano yoyote ya Palestine-Palestina ambayo yameidhinishwa na watu wa Palestina na yanaungwa mkono na makundi yote ya Palestina. Haki ya watu wa Palestina ya kujitawala lazima iheshimiwe,” Pezeshkian aliongeza.

Rais wa Iran pia alitoa mapendekezo ya Iran kuhusu suala la Palestina kwa ajili ya kuzingatiwa na kufanya maamuzi ya wanachama.

Alitoa wito kwa shirika la D-8 kuunda mpango wa msaada kwa ajili ya maendeleo na ujenzi wa Palestina, kuanzisha kikundi cha mawasiliano ili kushirikiana na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu katika kusitisha vita dhidi ya Gaza na kutoa misaada ya kibinadamu, na kuanzisha mfuko wa kujenga upya Gaza. na Lebanon.

Pezeshkian pia alihimiza shirika hilo kuunga mkono kutambuliwa kwa Israeli kama chombo cha ubaguzi wa rangi na kufanya kazi ya kufufua azimio nambari 3379 la Umoja wa Mataifa, huku likiunda kamati ya pamoja ya kisheria kusaidia Palestina katika hatua za kisheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuwashtaki maafisa wa Israeli kwa vifo vya zaidi ya watoto 17,000 wa Kipalestina.

Kwingineko katika matamshi yake, Rais wa Iran amesisitiza udharura wa kushughulikia hali ya wakimbizi na watu wasio na makazi, pamoja na ulazima wa usaidizi wa haraka wa kimataifa kwa Lebanon, ambayo iliteseka vibaya sana na uvamizi wa Israel katika miezi michache iliyopita.

Kuhusu mashambulio mabaya ya Israel dhidi ya miundombinu ya Syria, hususan jeshi lake, amesisitiza kuwa Iran inalaani vikali mashambulizi ya utawala huo kwenye miundombinu, mali na za nchi hiyo ya Kiarabu.

"Tunaeleza kusikitishwa kabisa na ukimya wa mashirika na vikao vya kimataifa, hasa Umoja wa Mataifa, kuhusu uchokozi wa utawala wa Israel na kukalia kwa mabavu ardhi ya Syria. Tunatoa wito wa kuondolewa kabisa kwa wavamizi na kurejeshwa kwa utulivu na usalama nchini,” Pezeshkian alisisitiza.

Israel ilianzisha vita vya mauaji ya kimbari huko Gaza mnamo tarehe 7 Oktoba 2023 na hadi  mashambulizi  hayo sasa yamesababisha vifo vya Wapalestina zaidi ya 45,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na wengine 107,244 kujeruhiwa. Maelfu zaidi pia wametoweka na inakisiwa kuwa wamekufa chini ya vifusi.

Jumuiya ya D-8 ya ushirikiano wa kiuchumi ambayo pia inajulikana kama Jumuiya ya Nchi 8 Zinazostawi ni shirika lililojikita katika kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi kati ya Bangladesh, Misri, Indonesia, Iran, Malaysia, Nigeria, Pakistan, na Uturuki.

captcha