
Chuo Kikuu cha Cairo kiliandaa hafla ya kuwaheshimu baadhi ya washiriki wa kipindi hicho, akiwemo Aya Abdel Rahman, mtangazaji wa programu hiyo na mhadhiri msaidizi katika Kitivo cha Elimu Maalumu cha chuo hicho, pamoja na Muhammad al‑Qalaji na Bilal Saif, washiriki wawili walioongoza katika mashindano.
Katika hafla hiyo, Sheikh Ashraf al‑Feel, mmoja wa wanazuoni wa Al‑Azhar, alisema kuwa kipindi cha Dawlat El‑Tilawah kimekuwa na nafasi muhimu katika jamii, kwani kimewapa watazamaji fursa ya kufufua kumbukumbu za enzi za kusikiliza sauti za maqurra wakubwa waliopamba historia ya usomaji wa Qur’ani Tukufu.
Kwa upande wake, Muhammad al‑Qalaji, mmoja wa washiriki bora wa kipindi hicho, alishukuru Chuo Kikuu cha Cairo kwa kuandaa hafla hiyo, akieleza kuwa alianza kuhifadhi Qur’ani akiwa na umri wa miaka minne, na baadaye kuhudhuria duru na masomo yaliyoendeshwa na maprofesa na masheikh mbalimbali wa Misri.
Naye Bilal Saif, mshiriki mwingine aliyeng’ara katika kipindi hicho, alisema kuwa alikamilisha hifdhi ya Qur’ani akiwa na umri wa miaka 15 katika mkoa wa Beni Suef, na baada ya kuhamia Cairo alijitahidi kujifunza qiraat za Qur’ani kwa kurejea kwa walimu mashuhuri ili kuboresha zaidi kiwango chake cha usomaji.
Kipindi cha Dawlat El‑Tilawah kinazalishwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Awqaf ya Misri na Shirika la United Media Services, kwa lengo la kubaini vipaji na maqurra mahiri kutoka mikoa mbalimbali ya nchi hiyo.
Kipindi hiki hurushwa kupitia vituo vya satelaiti vya Al‑Hayat, CBC, Al‑Nas, Misr Al‑Qur’an Al‑Karim, pamoja na jukwaa la “Watch It”, na hurushwa kila Ijumaa na Jumamosi saa 3:00 usiku (9:00 pm).
Mashindano haya yanatoa jumla ya zawadi ya pauni milioni 3.5 za Misri. Washindi wa nafasi ya kwanza katika vipengele vya qiraah (usomaji) na tajwid kila mmoja atapokea pauni milioni moja, sambamba na kurekodi Qur’ani Tukufu kwa sauti zao na kuitangaza kupitia kituo cha Misr Qur’an Karim.
Zaidi ya hayo, watapewa heshima ya kuongoza Swala ya Tarawehe katika Msikiti wa Imam Hussein (AS) wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, heshima kubwa inayothaminiwa sana katika ulimwengu wa Kiislamu, hususan miongoni mwa wapenzi wa Qur’ani.
Habari inayohusiana:
Jopo la majaji wa kipindi hiki linajumuisha wanazuoni na watu mashuhuri kutoka ulimwengu wa Kiislamu, akiwemo Hassan Abdel‑Nabi, Taha Abdel‑Wahab, Mostafa Hosny, na Taha Al‑Nuamani.
Vilevile, kipindi kimepambwa na wageni maalumu wakiwemo Osama al‑Azhari, Nazir Mohamed Ayyad, Ali Gomaa, Ahmed Nuaina, Abdel‑Fattah al‑Tarouti, Jaber al‑Baghdadi, mwanazuoni wa Uingereza Muhammad Ayoub Asif, pamoja na qari mashuhuri wa Morocco Omar al‑Qazabri.
Kipindi cha mwisho cha msimu wa kwanza kinatarajiwa kurushwa siku ya kwanza ya Ramadhani 2026, ambapo mshindi wa kwanza wa mashindano haya ya Qur’ani atatangazwa rasmi.
4333630