IQNA

Qatar kuzindua Kituo cha Qur'ani cha Saa 24 siku ya kwanza ya Mwezi wa Ramadhani

11:54 - February 17, 2026
Habari ID: 3481949
IQNA –Sambamba na kuonekana kwa mwezi mwandamo unaoashiria kuingia kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, watazamaji nchini Qatar na nje ya nchi hiyo watapata mwandani mpya wa kiroho.

Shirika la Vyombo vya Habari la Qatar (Qatar Media Corporation) limetangaza uzinduzi wa Kituo cha Qurani cha Qatar kuanzia siku ya kwanza ya Ramadhani ijayo, hatua inayopanua wigo wa vituo maalumu vya shirika hilo la utangazaji.

Kituo hicho kipya cha televisheni kitajikita katika kurusha tilawa za Qurani Tukufu saa 24, kama sehemu ya juhudi za kukuza vyombo vya habari vya kidini vyenye mwelekeo na kuimarisha maudhui maalumu sambamba na Dira ya Kitaifa ya Qatar 2030.

Mkurugenzi Mtendaji wa Qatar Media Corporation, Sheikh Khalid bin Abdulaziz bin Jassim Al-Thani, alielezea mpango huo kuwa ni hatua ya kimkakati ndani ya mkakati wa shirika wa kupanua vituo vya maudhui mahsusi.

Alisema kituo hicho kinaakisi dhamira ya shirika katika kuwasilisha maudhui ya Qurani yenye ubora wa hali ya juu, kuchangia kueneza Qurani Tukufu kupitia majukwaa mbalimbali ya vyombo vya habari, na wakati huo huo kuimarisha utambulisho wa kitaifa na maadili ya jamii.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji huyo, timu za maandalizi zimefanya kazi kwa umakini ili kuhakikisha utayari wa kiutendaji chini ya mpango madhubuti, ikiwa ni pamoja na uchaguzi makini wa tilawa, zilizopitia tathmini za kiufundi na za kidini ili kuhakikisha ubora na usahihi.

Pia, maandalizi ya taswira na uzalishaji wa picha yamefanywa kwa namna inayolingana na muundo wa kituo.

Kituo hicho kitatoa kipaumbele maalumu kwa qari wa Kiqatar, kikionyesha mchango wa nchi hiyo katika kuhudumia Qurani Tukufu na kutambulisha sauti bora za kitaifa.

Mkurugenzi wa Qatar TV, Ali Saleh Al Sada, alisema kituo hicho kipya kitakuwa nyongeza yenye thamani kubwa katika mtandao wa vituo vya televisheni na redio vya shirika hilo.

Alibainisha kuwa vipindi vitajumuisha tilawa endelevu za Qurani, khatma kamili, pamoja na urushaji wa moja kwa moja wa Swala za Tarawehe kila siku katika mwezi wa Ramadhani, kwa kuzingatia viwango vya juu vya sauti na picha kwa watazamaji wa ndani na nje ya Qatar.

Holy Quran

Kituo hicho kitarushwa kupitia setilaiti mbili zinazofunika Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini: Arabsat (Badr 8) na Eutelsat (E7WA). Pia kitapatikana kwa utazamaji wa moja kwa moja mtandaoni kupitia programu ya simu ya Tabie QMC.

Maafisa walisema uzinduzi huo ni matokeo ya ushirikiano wa idara mbalimbali ndani ya shirika, pamoja na uratibu na Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu.

Upigaji picha wa vipindi vya kituo hicho umefanyika katika misikiti mbalimbali nchini Qatar, ili kuonesha utambulisho wa usanifu wa Kiislamu wa nchi hiyo.

Abdullah Mohammed Al Buainain, Msimamizi wa Redio ya Qurani ya Qatar, alisema kituo hicho cha redio kimeweka rasilimali zake zote kusaidia mradi huo, ikiwa ni pamoja na kutoa tilawa zilizorekodiwa za maqari wa Kiqatar kwa ajili ya kurushwa kupitia redio na kituo kipya cha televisheni.

Uzinduzi huo ni sehemu ya mkakati mpana wa upanuzi wa vyombo vya habari kwa uwiano, unaoangazia mchango wa Qatar katika kuhudumia Qurani Tukufu, hususan katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mwezi wa Ramadhani, mwezi wa tisa katika kalenda ya Kiislamu, unatarajiwa kuanza Jumatano au Alhamisi nchini Qatar, kulingana na kuonekana kwa mwezi mwandamo.

3496447

captcha