IQNA

Uchambuzi wa Mapambano Dhidi ya Uzayuni katika Qur’ani/1

Simulizi ya Mbinguni na ya Kidunia kuhusu Mapambano ndani ya Qur’ani Tukufu

16:40 - March 06, 2026
Habari ID: 3482020
IQNA-Qur’ani Tukufu, pamoja na kuonyesha takwimu na uchambuzi wa mambo kwa mtazamo wa kidunia, pia inatuwekea mbele mtazamo mwingine wa kutafakari kuhusu mapambano.

Ni simulizi au riwaya ya mbinguni inayotendeka sambamba na sunna na kanuni za Mwenyezi Mungu, nayo huwa ufunguo wa kuelewa mabadiliko ya nyakati na siri ya kusimama imara kwa Mhimili wa Muqawama (mapambano ya Kiislamu) dhidi ya dhulma.

Katika mfululizo wa makala kadhaa, tunakusudia kuchambua matukio ya karibuni, hasa mashambulizi ya kikatili ya Marekani na Wazayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuyatazama katika mwanga wa aya za Qur’ani Tukufu.

Kila tukio linaweza kusimuliwa kwa mitazamo miwili: simulizi ya kidunia na simulizi ya mbinguni. Kwa mfano, katika kuchambua vita, kuna simulizi ya kidunia ambayo sehemu yake huonekana katika takwimu; kama vile ni makombora mangapi yalirushwa au ni maadui wangapi waliuawa na kujeruhiwa. Simulizi hii ya kidunia ina mantiki na kanuni zake.

Qur’ani Tukufu pia inaashiria jambo hili pale inaposema:

“Na waandalieni kadiri muwezavyo nguvu na farasi wa vita.” (Al‑Anfal: 60)

Maana yake ni kwamba kuingia katika uwanja wa mapambano kunapaswa kuandamana na mkakati, mantiki na vifaa vinavyohitajika; wala haifai mtu kujitosa bila tahadhari au bila maandalizi.

Hata hivyo, hili ni sehemu tu ya simulizi. Pembeni yake kuna pia simulizi ya mbinguni. Simulizi hii ya mbinguni ina mifano mingi ndani ya Qur’ani Tukufu.

Mfano ulio hai mbele yetu ni  mwamko wa Qiyamu ya ‘Ashura na mwenendo wa Imam Husayn (AS). Katika simulizi ya kidunia, yeye pamoja na maswahaba wake waliuawa shahidi na Ahlul‑Bayt wake au watu wa nyumba yake wakachukuliwa mateka. Lakini katika simulizi ya mbinguni, fikra na ujumbe wa  Imam Hussein (AS) ambaye pia ni maarufu Sayyid al‑Shuhadaa yaani bwana wa Mashahidi ukawa jahazi la wokovu na uongofu kwa Umma wa Kiislamu.

Katika mkondo wa matukio ya karibuni nchini Iran, licha ya mashaka, majaribu na mashahidi ambao damu yao imetolewa kwa ajili ya nchi hii, ni lazima pia kuzingatia simulizi ya mbinguni.

Ingawa pande zote mbili, simulizi ya kidunia na ile ya mbinguni, zinatoa bishara ya ushindi na nusra kwa safu ya Uislamu, lakini kile kinachowatia matumaini zaidi watu wa imani na kinachoonekana kuwa cha uhakika zaidi ni kutafakari sunna za Mwenyezi Mungu na simulizi ya mbinguni ya mapambano.

3496650

captcha