IQNA

Mashindano ya Kwanza ya Kitaifa ya Kuhifadhi Qur’ani kwa Vijana Yazinduliwa Kosovo

14:53 - April 18, 2026
Habari ID: 3482148
IQNA – Mashindano ya kwanza ya kitaifa ya kuhifadhi Qur’ani kwa vijana wenye umri kati ya miaka 12 hadi 30 yameanza nchini Kosovo siku ya Ijumaa.

Washiriki 100 kutoka miji mbalimbali ya Kosovo wanashindana katika sehemu mbili: ya wanaume na ya wanawake.

Wanachuana kupata nafasi za juu katika ngazi tatu: kuhifadhi Juzuu 10 za Qur’ani Tukufu, kuhifadhi Juzuu 5, na kuhifadhi Juzuu 2.

Hatua ya mwisho na sherehe ya kufunga zinatarajiwa kufanyika Jumapili, tarehe 20 Aprili, katika mji mkuu wa Kosovo, Pristina, kwa uwepo wa viongozi wa serikali, wana jamii na watu mashuhuri wanaoonyesha umuhimu wa tukio hili la Qur’ani.

Mashindano haya yanawalenga vijana na watoto baleghe wenye umri kati ya miaka 12 na 30, wakiwemo wanafunzi wa vituo vya kuhifadhi Qur’ani, wanafunzi wa taasisi za kidini, na wale wa shule za kawaida.

Kwa mujibu wa waandaaji, malengo ya mashindano haya ni kuimarisha utamaduni wa kuhifadhi Qur’ani miongoni mwa vijana, kugundua vipaji vya Qur’ani, kukuza uwezo wa vijana katika kuhifadhi na kusoma kwa tartiil, kuwatia moyo watoto Waislamu wa Kosovo kuimarisha usomaji wa Qur’ani, na kuendeleza moyo wa ushindani mwema katika nyanja za Qur’ani.

Tukio hili linafanyika kama sehemu ya juhudi za kuimarisha programu za elimu zinazohusiana na kuhifadhi Qur’ani miongoni mwa vijana, kuimarisha maadili tukufu ya Kiislamu, na kuwaunganisha vijana na kizazi cha baleghe na Qur’ani Tukufu.

Kosovo ni nchi isiyo na bahari katika Ulaya ya Kusini-Mashariki yenye utambuzi wa kidiplomasia wa kiasi. Inapakana na Albania kusini-magharibi, Montenegro magharibi, Serbia kaskazini na mashariki, na Masedonia Kaskazini kusini-mashariki.

Kosovo ina wakazi wasiofikia milioni mbili. Takriban asilimia 88 ni wa kaumu ya Waalbania, 7 % Waserbia na wengine mchanganyiko wa Waturuki na vikundi vidogo.

Upande wa dini, Waalbania wengi ni Waislamu na Waserbia wengi ni Wakristo Waorthodoksi lakini kuna pia Waalbania Wakatoliki na Waorthodoksi, pia Waserbia Waislamu kadhaa. Kwa jumla, Waislamu ni 95.6% na Wakristo 3.7% (Wakatoliki 2.2%, Waorthodoksi 1.5%).

3497128


 

3497128

Kishikizo: qurani tukufu kosovo
captcha