IQNA

Madada wa Kosovo wawafundisha mamia ya watoto Qur’ani

15:14 - June 01, 2026
Habari ID: 3482311
IQNA – Kwa kuanzisha akademia ya Qur’ani, madada wawili mjini Pristina, mji mkuu wa Kosovo, wameweza kuwafundisha mamia ya watoto namna ya kusoma na kuhifadhi Qur’ani Tukufu kupitia miaka yao ya juhudi na bidii.

Pia wamejumuisha sanaa, shughuli za ubunifu na shughuli za kijamii ndani ya programu zao za elimu.

Madada hao wawili, Renita na Fatima Nitai, wamejitokeza kuwa vielelezo mashuhuri katika elimu ya Kiislamu. Wameigeuza shauku yao kwa Qur’ani Tukufu kuwa mradi wa elimu wenye athari kubwa, uliosaidia kuwalea na kuwaelimisha mamia ya watoto, pamoja na kuinua kizazi kipya cha mahafidhi wa Qur’ani na wapenda Kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Mafanikio haya hayakupatikana kwa bahati nasibu, bali yamekuja kupitia miaka ya masomo na umahiri katika taaluma za Qur’ani, jambo lililopelekea kuanzishwa kwa Akademia ya “Wahifadhi Wadogo wa Qur’ani”, ambayo sasa imekuwa miongoni mwa juhudi mashuhuri zaidi za Qur’ani kwa watoto nchini Kosovo.

Madada hao walikulia katika mazingira ya Qur’ani na wakaanza safari yao ya elimu katika Shule ya Upili ya Kiislamu ya Alaeddin mjini Pristina, iliyo chini ya Jumuiya ya Kiislamu ya Kosovo. Huko walifanya vyema katika masomo ya Qur’ani na kuiwakilisha Kosovo katika mashindano ya Qur’ani ya ndani na ya kikanda.

Waliendelea na masomo yao katika Kitivo cha Masomo ya Kiislamu mjini Pristina na kupata shahada za uzamili. Mwaka 2024, walifikia moja ya hatua zao muhimu zaidi za kielimu walipopata ijaza ya kisomo cha Qur’ani kutoka Chuo Kikuu cha Al-Azhar.

Kwa sasa, madada hao wanaendelea na safari yao ya taaluma kwa kufuatilia shahada za uzamivu, jambo linalodhihirisha kujitolea kwao kuunganisha elimu ya nadharia na utekelezaji wa vitendo.

Baada ya miaka ya masomo na mafunzo, waliasisi Akademia ya “Wahifadhi Wadogo wa Qur’ani” mjini Pristina chini ya usimamizi wa Jumuiya ya Kiislamu ya Kosovo. Akademia hiyo ni jukwaa maalumu la kielimu la kuwafundisha watoto namna sahihi ya kusoma na kuhifadhi Qur’ani Tukufu, kwa kutumia mitaala inayozingatia tofauti za umri na uwezo wa kila mtoto.

Akademia hiyo imefanikiwa kuvutia idadi kubwa ya watoto na inatoa ufuatiliaji wa mtu mmoja mmoja pamoja na programu mbalimbali za elimu zinazosaidia kuimarisha uhusiano wao na Qur’ani Tukufu na kukuza maendeleo yao kwa ujumla.

Linalolitofautisha zaidi jambo la masista hawa wawili ni kuwa mradi wao haujajikita katika kuhifadhi na kusoma Qur’ani pekee. Bali umejengwa juu ya kuunganisha Qur’ani Tukufu na mwenendo wa kila siku pamoja na maadili ya kivitendo, kwa kupandikiza kwa watoto dhana za ukweli, uaminifu, kuwatii wazazi, ushirikiano na kuwajibika.

Pia wameingiza sanaa na shughuli za ubunifu ndani ya mchakato wa elimu kupitia mashindano ya uchoraji, kazi za mikono na programu za kitamaduni zinazowasaidia watoto kuamiliana na maadili ya Qur’ani kwa namna ya vitendo na yenye kuwavutia.

Juhudi za madada hawa hazikuishia darasani pekee, bali zimeenea hadi kuibadilisha elimu ya Qur’ani kuwa miradi ya kijamii yenye matokeo ya moja kwa moja. Watoto hushiriki katika kazi za hisani, kutembelea familia zenye uhitaji, na miradi inayokuza maadili ya mshikamano, uzalendo wa kijamii na kuitumikia jamii.

Mtindo huu umefanya maadili ya Qur’ani wanayojifunza watoto yageuke kuwa vitendo vya kila siku vinavyoonekana wazi, jambo lililopata kuthaminiwa sana katika jamii.

Mpango huu ni kielelezo cha mafanikio kwa wanawake wa Kiislamu nchini Kosovo. Wameunganisha elimu ya juu ya kitaaluma, masomo ya Kiislamu, kazi ya ufundishaji na juhudi za kijamii, na hivyo kuigeuza elimu ya Qur’ani kuwa mradi wa vitendo wa kulitumikia kizazi kipya.

Kwa sababu ya mafanikio haya, Akademia ya “Wahifadhi Wadogo wa Qur’ani” imekuwa mfano unaong’aa wa uwezo wa juhudi za elimu ya Kiislamu katika kulea kizazi kinachounganisha hifdhi ya Qur’ani na maadili mema, hisia ya kuwajibika kwa jamii, na utambulisho wa Kiislamu.

3497667

Kishikizo: kosovo qurani tukufu
captcha