Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na tovuti ya Muslims Around the World na kunukuliwa na IQNA, darsa hizi zinazoendeshwa chini ya nembo ya “Tarbiyah kwa Muhaba na Uongozi wa Kiubunifu,” zinatoa fursa adhimu kwa watoto kujenga mafungamano ya dhati na Kitabu Kitukufu cha Mwenyezi Mungu na kukuza malezi yao katika mazingira yaliyosheheni elimu, akhlaq ya Kiislamu na stadi za maisha.
Katika kipindi chote hiki cha likizo, chuo hiki kinashuhudia mwamko mkubwa na mahudhurio ya kila siku ya watoto ambao nyoyo zao zimefungamana na Qur’an, huku sauti zao nyororo za usomaji zikivuma na kupendezesha madarasa. Taswira hii inadhihirisha wazi mafanikio makubwa ya programu hii katika kutumia vyema wakati wa likizo kulea kizazi kilichoshikamana na Wahyi; kizazi ambacho hakisomi tu aya, bali kinayaishi mafundisho yake kupitia matendo na shughuli mbalimbali za kijamii na kielimu zilizoandaliwa kwa usimamizi thabiti.
Programu hii inalenga kufundisha Qur’ani Tukufu kwa kutumia mbinu za kisasa zinazoendana na rika mbalimbali za watoto, ambapo wanafunzi hufundishwa usomaji sahihi (Tajweed), hifdhi ya aya, pamoja na kufundishwa misingi na maadili yaliyomo ndani ya Qur’ani Tukufu.
Uongozi wa chuo hicho umesisitiza kuwa darsa hizi za kiangazi si sehemu tu ya kupoteza wakati wa ziada, bali ni chemchemi ambapo elimu inakutana na muhaba, na malezi yanajengwa juu ya msingi wa ubunifu; mazingira yanayomuwezesha mtoto kuondoka na kumbukumbu nzuri na kuchukua hatua madhubuti kuelekea maisha yanayoongozwa na misingi ya Qur’ani (Mtindo wa Maisha wa Kiqur’ani).
Shughuli za kila siku za mradi huu zinajumuisha mtaala mpana wenye masomo ya Qur’an, michezo ya kielimu, warsha za kuamsha fikra, kazi za makundi, na mashindano ya motisha yanayoambatana na zawadi mbalimbali. Hali hii inajenga mazingira changamfu ya kujifunza yanayomfanya mtoto apende masomo yake huku akipandikizwa maadili mema ya Kiislamu kwa njia ya vitendo.
Malengo ya darsa hizi yanakwenda mbali zaidi ya kuhifadhi na kusoma tu aya za Mwenyezi Mungu; yanahusisha pia ujenzi wa shakhsia imara ya mtoto, kukuza roho ya ushirikiano, nidhamu, kujiamini, na kuimarisha uhusiano wa karibu kati ya mtoto, msikiti, familia na jamii yake ya Kiislamu.
Mradi huu ni thibitisho tosha kwamba kila neno jipya analojifunza mtoto, kila aya anayoisoma, na kila tabia njema anayoijenga, ni hatua muhimu kuelekea kujenga moyo uliosheheni nuru ya Qur’an na unaofuata mfumo wa maisha wa Kiislamu. Hili ndilo lengo kuu la chuo hiki katika kuandaa kizazi chenye upeo wa maarifa, tabia njema (akhlaq), na mwenendo wa Kiqur’ani.
3498264