IQNA

Mashindano ya 11 ya Kimataifa ya Qur’ani Yaanza Diyarbakir, Uturuki

14:12 - April 22, 2026
Habari ID: 3482158
IQNA – Toleo la 11 la mashindano ya kimataifa ya kusoma na kuhifadhi Qur’ani Tukufu nchini Uturuki limeanza rasmi siku ya Jumatatu.

Tukio hilo la kimataifa la Qur’ani limefunguliwa katika mji wa Diyarbakir, mashariki mwa nchi hiyo, kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Ilkha.

Sherehe ya ufunguzi imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa jengo la Salahuddin Ayyubi, lililopo wilayani Inişehr katikati ya Diyarbakir. Idadi kubwa ya wageni, pamoja na mahafidh na washiriki kutoka mataifa mbalimbali, walihudhuria hafla hiyo.

Katika mashindano haya, wawakilishi 44 kutoka nchi 36 kama vile isri, Urusi, Iran, Tajikistan, Denmark, Malaysia, New Zealand na Palestina  wanashiriki. Washiriki 12 wanashindana katika kipengele cha usomaji wa Qur’ani, huku wengine 32 wakishiriki katika kipengele cha hifdhi (kuhifadhi Qur’ani Tukufu kikamilifu).

Hafla ya utoaji wa tuzo imepangwa kufanyika Aprili 29 katika Ikulu ya Rais jijini Ankara, mji mkuu wa Uturuki, kwa uwepo wa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan.

Miongoni mwa waliohutubia katika hafla ya ufunguzi ni Celal Büyük, Mufti wa Diyarbakir; Osman Işın Yürek, Mwenyekiti wa Kamati ya Qur’ani na Usomaji katika Kurugenzi ya Masuala ya Dini ya Uturuki; Mustafa Şentop, Spika wa Bunge la 29 la Uturuki; Hafidh Osman Şahin, Naibu Mkuu wa Masuala ya Dini; pamoja na Sayyid Yaz, mwakilishi wa Chama cha Haki na Maendeleo (AKP) Diyarbakir, na viongozi wengine.

Katika hotuba yake, Şentop alisema kuwa hifzi ya Qur’ani Tukufu imeutofautisha Umma wa Kiislamu katika historia yote. “Kitabu hiki hakijaandikwa tu, bali pia kimehifadhiwa ndani ya nyoyo za watu,” alisema.

Akisisitiza kuwa karibu kila familia ina mhifadhi wa Qur’ani, alieleza kwamba hifzi ni daraja tukufu na heshima kubwa. Aliwapongeza washiriki wa mashindano hayo na kuwasihi wasiisahau Qur’ani katika dua na ibada zao.

Naye Hafidh Osman Şahin, Naibu Mkuu wa Masuala ya Dini, aliwashukuru waandaaji na kueleza kuwa Qur’ani Tukufu ni kitabu cha maisha, ni neno lililo bora zaidi, ni kamba madhubuti ya Mwenyezi Mungu, na ni rehema pamoja na shifa.

Aliongeza kuwa kuisoma, kuihifadhi na kuisikiliza Qur’ani ni ibada, na kwamba kuishi kwa mujibu wa mafundisho yake ndilo lengo la juu kabisa.

Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa kuzingatia utekelezaji wa mafunzo ya Qur’ani katika maisha ya kila siku.

3497181

captcha