
Idara hiyo imesema kuwa programu na shughuli hizo zinatekelezwa kwa ushiriki wa nchi 27, kwa lengo la kuimarisha na kuhuisha misingi ya umoja na uadilifu; taarifa hiyo imenukuliwa na Shirika Rasmi la Habari la Iraq (INA).
Mji mtukufu wa Najaf utashuhudia makumi ya matukio ya Qur’ani na ya kitamaduni, pamoja na onesho kubwa zaidi la tamthilia ya mitaani litakaloweza kuchukua watazamaji 5,000 katika kipindi cha Wiki ya Kimataifa ya Ghadir.
Kadhalika, bendera ya Ghadir itainuliwa katika takriban maeneo 150 na mikusanyiko ndani na nje ya Iraq katika wiki hiyo
Haider Rahim, mkuu wa kitengo cha habari cha Idara ya Mfawidhi au Msimamizi wa wa Haram Tukufu ya Imam Ali (AS) , amesema katika mkutano na waandishi wa habari leo kuwa Wiki ya Kimataifa ya Ghadir ni miongoni mwa matukio makuu zaidi ya kidini na kitamaduni yanayoandaliwa na Ustana katika mnasaba wa ‘Id al-Adha.
Amebainisha kuwa lengo la tukio hili ni kusimamisha na kuimarisha maadili ya Wilayah (uongozi/uwali), umoja, uadilifu, na kuunganisha nyoyo na maisha ya Imam Ali (AS), kupitia programu mbalimbali za kidini, kitamaduni, kisanii, za kijamii, na za huduma.
Amesema Mradi wa Kuinua Bendera ya Ghadir utashuhudia upanuzi wake mkubwa zaidi mwaka huu tangu kuanzishwa kwake; akieleza kuwa idadi ya maeneo ya kuinua bendera imeongezeka kutoka takriban 90 katika miaka iliyopita hadi karibu 150 mwaka huu.
Ameongeza kuwa nchi zinazoshiriki ni pamoja na Uingereza, Uswidi, Denmark, Ujerumani, Norwei, Ufini, Hispania, Uholanzi, Ubelgiji, Romania, Jamhuri ya Czech, Ufaransa, Austria, Iran, India, Pakistan, Australia, Lebanon, Thailand, Uturuki, Indonesia, Saudi Arabia, China, Kenya, Nigeria, Ivory Coast, na Misri.
Tukio la Ghadir, au ‘Eid ul Ghadir, aghalabu huadhimishwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia duniani kote kila mwaka.
Ni miongoni mwa ‘Eid na sikukuu za furaha zilizo muhimu katika Ushia na huadhimishwa tarehe 18 Dhul-Hijjah katika kalenda ya Hijri ya mwezi, ambayo mwaka huu huangukia Alhamisi, Juni 4.
Ghadir ilikuwa siku ambayo, kwa mujibu wa riwaya na taarifa, Mtume Mtukufu (SAW) alimteua Ali ibn Abi Talib (AS) kuwa khalifa wake na Imam baada yake, kufuatia amri ya Mwenyezi Mungu.
3497666