IQNA

Hamas: Kufungwa kwa Msikiti wa Ibrahimi ni ukiukaji wa wazi wa uhuru wa ibada

15:38 - May 30, 2026
Habari ID: 3482300
IQNA – Hatua ya utawala wa Israel ya kuufunga Msikiti wa Ibrahimi katika mji wa Al-Khalil (Hebron) ni ukiukaji wa wazi wa uhuru wa kuabudu na wa haki ya wananchi wa Palestina, harakati ya muqawama ya Palestina, Hamas, imesema.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Ijumaa, Hamas ililaani hatua hiyo, ikisema ni uhalifu mpya na shambulio la wazi dhidi ya moja ya maeneo matukufu ya Kiislamu. Harakati hiyo ilisema hatua hiyo ni ukiukaji wa wazi wa uhuru wa ibada na wa haki ya Wapalestina kufikia maeneo yao matukufu na kutekeleza ibada zao.

Hamas ilionya dhidi ya kuongezeka kwa ukiukaji wa Israel dhidi ya maeneo matukufu ya Kiislamu, pamoja na kuendelea kwa sera zake za “kuyahudisha” (Judaization) na kuwakandamiza kwa utaratibu Wapalestina, katika kile ilichokitaja kuwa ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuanzisha “uhalisia mpya” unaolenga utambulisho wa Kiarabu na Kiislamu wa Msikiti wa Ibrahimi na maeneo yote matukufu.

Taarifa hiyo imebaini kuwa" “Sera hizi za uchokozi na za kuyahudisha hazitafanikiwa kubadili utambulisho wa Msikiti wa Ibrahimi au kudhoofisha haki ya watu wetu waliodumu imara juu yake. Utabaki kuwa msikiti wa Kiislamu kikamilifu, na watu wetu wataendelea kushikamana na haki zao na misimamo yao thabiti na kuyalinda maeneo yao matukufu, bila kujali gharama.”

Hamas imeitaka jumuiya ya kimataifa, Umoja wa Mataifa na taasisi zake husika kuchukua hatua za haraka na zenye ufanisi ili kusitisha ukiukaji huu mkubwa, na kuchukua hatua za kuzuia dhidi ya kile ilichokiita serikali ya adui ya Kizayuni yenye mielekeo ya kifashisti, ambayo inazidisha mashambulizi yake dhidi ya ardhi ya Palestina, watu wake na maeneo yake matukufu.

Vilevile, Hamas iliwaomba Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi kwa ujumla, na hasa wa mji wa Al-Khalil hususan, waongeze uwepo wao na ribat (kusimama imara/kuendeleza ulinzi na uwepo wa kidini) katika Msikiti wa Ibrahimi, na wakabiliane na mipango yote ya Israel inayolenga “kuyahudisha” na kuweka udhibiti juu yake. 

3497648

Kishikizo: ibrahimi msikiti
captcha