
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amewaambia waandishi wa habari kwamba: “Asilimia mia moja ya ardhi ya Gaza ni ya watu wa Palestina.”
Dujarric ameongeza kuwa: “Hilo ndilo tunalotaka kuliona, na tumekuwa tukiitaka Israel ijiondoe kutoka katika uvamizi wake kuanzia kile kinachoitwa mstari wa njano, na huo utaendelea kuwa msimamo wetu.”
Kauli zake zilikuja baada ya Netanyahu kusema Alhamisi kwamba Israel kwa sasa inadhibiti takriban asilimia 60 ya Ukanda wa Gaza na inapanga kuongeza kiwango hicho hadi asilimia 70. Hakutoa maelezo kuhusu namna eneo hilo la ziada litakavyotekwa.
Jeshi la Israel lilitangaza mwezi Oktoba mwaka jana kwamba lilikuwa linadhibiti asilimia 53 ya Gaza baada ya kujipanga upya katika kile kinachoitwa “mstari wa njano”, chini ya awamu ya kwanza ya mpango uliopendekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump wa kumaliza vita katika eneo hilo.
Mpangilio huo ulitarajiwa kushuhudia kujiondoa zaidi kwa majeshi ya Israel katika awamu ya pili iliyoanza Januari.
“Mstari wa njano” ni eneo la muda la utenganisho mashariki mwa Gaza linalogawa maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa jeshi la Israel na maeneo ambayo Wapalestina wanaruhusiwa kubaki.
Hata hivyo, vyanzo vya Kipalestina vinaonya kwamba mpaka huo umekuwa ukisogezwa taratibu kuelekea magharibi katika miezi ya karibuni.
Bassem Naim, mwanachama mwandamizi wa harakati ya mapambano ya Kipalestina ya Hamas, amesema Israel imesukuma mstari huo mbele kwa ziada ya asilimia 8 hadi 9 ndani ya Gaza, na hivyo kufanya eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel kuvuka asilimia 60.
Tangu kuanzisha mashambulizi yake ya mauaji ya halaiki dhidi ya Gaza tarehe 7 Oktoba 2023, Israel imewaua zaidi ya Wapalestina 72,000 na kuwajeruhi wasiopungua 172,000 wengine, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Vita vya Israel pia vimeharibu kwa kiasi kikubwa miundombinu ya kiraia ya Gaza, ikiwemo hospitali, shule, viwanja vya michezo, mitambo ya umeme, mitandao ya maji na vitongoji vya makazi katika eneo lote lililowekwa chini ya mzingiro.
Uharibifu huo mkubwa pamoja na mzingiro unaoendelea umesababisha sehemu kubwa ya wakazi wa Gaza kuyahama makazi yao, huku Wapalestina wakibaki wamenaswa ndani ya eneo hilo lililozingirwa na kutegemea kwa kiwango kikubwa misaada ya kibinadamu inayoingia kwa idadi ndogo sana.
3497643