IQNA

Mwanazuoni: Kurudisha Hija kwenye Mkondo wa Kiibrahimu ni Suluhisho kwa Ulimwengu wa Kiislamu

17:51 - May 29, 2026
Habari ID: 3482293
IQNA – Mwanazuoni mmoja wa Iran amesema kuwa Bara’ah min al-Mushrikin (kujivua na kujitenga na washirikina) ndiyo nyenzo bora zaidi ya kuifufua Hija ya Kiibrahimu.

Akizungumza katika mahojiano na IQNA, Hujjat al-Islam Davoud Hosseini, mkurugenzi wa Idara ya Maadili katika Taasisi ya Utafiti wa Hija na Ziara, amesema kuwa Hija ya Kiibrahimu, iliyoasisiwa na Nabii Ibrahim (AS) na kuendelezwa na Mtume Muhammad (SAW), inaweza kuwa chombo cha kutatua matatizo na kuleta ufumbuzi kwa ulimwengu wa Kiislamu iwapo itarejeshwa kwenye mkondo wake wa asili.

Amebainisha kuwa miongoni mwa istilahi ambazo Imam Khomeini (RA) aliingiza katika fasihi ya kisiasa ya Hija ni “Bara’ah min al-Mushrikin” na “Hija ya Kiibrahimu.”

Amesema: “Suala hili, yaani Hija ya Kiibrahimu na sifa zake, pamoja na kujivua na washirikina, ni miongoni mwa maelekezo yaliyosisitizwa sana katika Qur’ani Tukufu.”

Alifafanua kuwa Hija ya Kiibrahimu ni Hija ambayo, mbali na ibada ya mtu binafsi, pia huibua na kuchambua vipengele vya kijamii na kisiasa, sambamba na matatizo na masuala yanayowakabili Waislamu.

Ameongeza kuwa:  “Tofauti na Umra, ambayo inaweza kufanywa katika msimu wowote, Mwenyezi Mungu ameifanya Hija kuwa faradhi katika wakati maalumu na kwa matendo maalumu, ili Waislamu wote watekeleze ibada hii kwa pamoja na bega kwa bega. Hili linaweka wazi kwamba, mbali na kipengele cha ibada ya mtu binafsi, kulikuwepo pia malengo mengine yaliyokusudiwa. Mbali na ibada binafsi, Waislamu wanapaswa pia kuzingatia masuala mengine ndani ya mkusanyiko huu mkubwa; matatizo ya jamii ya Kiislamu, mahitaji yake, na kila jambo linalochangia maendeleo ya jamii ya Kiislamu yapaswa kupewa uzito. Mambo haya yanaonesha kwamba, mbali na masuala ya ibada, Uislamu pia umeweka mbele malengo ya kijamii na kisiasa, na Hija imeshariishwa kwa sifa hizo.”

Hujjat al-Islam Hosseini ameongeza kuwa kama Hija ingekuwa ni ibada ya mtu binafsi pekee, basi ingeweza kuamrishwa, kama ilivyo Umra, itekelezwe wakati wowote mtu anapopata fursa.

Amesema pia kuwa: “Kwa hiyo Hija haina upande wa mtu binafsi pekee, bali ina vipengele vingine pia; na miongoni mwa vilivyo muhimu zaidi ni kipengele cha Bara’ah min al-Mushrikin, kwa maana kwamba Waislamu wanapaswa kujitenganisha kisera na maadui, watambue mipango yao ovu, wafahamu malengo yao na wakabiliane nayo. Kwa sababu hiyo, tunasema kwamba Hija, mbali na kuwa na upande wa kidini, pia ina upande wa kisiasa, na upande huo wa kisiasa hujidhihirisha katika kujivua na washirikina. Tukiliacha pembeni eneo hili, Hija itageuka kuwa ibada tupu isiyo na athari katika mustakbali wa Waislamu; yaani mtu anaenda, anatekeleza ibada na anarudi, bila kuwa na uelewa wa hatima na masuala ya Waislamu.”

Aliendelea kusema kuwa Imam Khomeini (R.A.) aliibua suala la Hija ya Kiibrahimu kwa sababu Nabii Ibrahim (A.S.) aliweka msingi mkuu wa dini yake ya Hanif katika kupambana na masanamu na ushirikina, na pia kupambana na washirikina na makafiri.

Aidha amebaini kuwa:  “Kwa sababu hiyo, Hija ya Kiibrahimu ilipendekezwa, na ndani yake kipengele cha kuondoa ushirikina na kupambana na washirikina kina umuhimu wa pekee. Ili kulifanya jambo hili litimie na kuirudisha Hija kwenye nafasi yake ya asili, pamoja na kuwafanya Waislamu wauelekee upande wa kisiasa wa Hija, utakaso wa nafsi na uhusiano wa mahujaji na Mwenyezi Mungu pia vina umuhimu mkubwa. Hata hivyo, Waislamu wanapaswa pia kuwa na uhusiano wa karibu baina yao, wafahamu matatizo ya wenzao, na wafikirie hatima yao ya pamoja, jambo ambalo ni miongoni mwa vipengele muhimu vya Hija. Kwa hivyo, ili kufikia lengo hili, ni lazima tuiokoe Hija kutoka katika mtazamo wa upande mmoja tu.”

Amendelea kueleza kuwa ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kutambua kwamba Hija ndiyo sehemu bora zaidi na jukwaa muhimu zaidi ambapo wawakilishi wa Waislamu kutoka pande zote za ulimwengu wa Kiislamu, na hata kutoka nchi zisizo za Kiislamu, hukutana pamoja, huelewana kuhusu masuala yao, husikilizana kuhusu matatizo yao, na hubadilishana mawazo ili kupata ufumbuzi.

Mwanazuoni huyo mwandamizi wa Kiislamu amesema kuwa" “Kisha hurudi katika miji na nchi zao na kuwafikishia wengine yale waliyoyasikia, huyasambaza na kupendekeza njia za ufumbuzi. Ikiwa upande huu wa Hija utazingatiwa, utakuwa msaada mkubwa mno kwa Umma wa Kiislamu, na ulimwengu wa Kiislamu hautabaki tena katika hali ya kutengwa na kutokujali.”

3497627

captcha