IQNA

Wapalestina wajaza viwanja vya Msikiti wa Al-Aqsa wakati wa Eid

15:02 - May 27, 2026
Habari ID: 3482290
IQNA – Maelfu ya waumini wa Kiislamu wameadhimisha swala ya Eid al-Adha katika Msikiti Mtukufu wa Al-Aqsa, katika mji mtakatifu wa Al-Quds, siku ya Jumatano.

Viwanja vinavyozunguka Msikiti wa Al-Aqsa vilikuwa vimefurika waumini Wapalestina waliofika kutekeleza ibada hiyo ya swala ya Eid.

Eid al-Adha ni kumbukumbu ya utiifu na utayari wa Nabii Ibrahim (AS) wa kumtoa mwanawe kama sadaka kwa amri ya Allah (SWT). Katika siku hii, Waislamu huchinja wanyama kwa ajili ya kumbukumbu ya sadaka ya Nabii Ibrahim, na nyama hiyo hugawiwa kwa mafaqiri na wahitaji katika jamii, ikiwa ni ishara ya ukarimu na umoja.

Sherehe za Eid al-Adha za mwaka huu, moja ya sikukuu muhimu zaidi katika kalenda ya Kiislamu,  zimeingia huku kukiwa na ukiukwaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya kusitisha vita unaofanywa na utawala wa Kizayuni, ambao umekuwa ukitekeleza mauaji ya kimbari huko Gaza tangu Oktoba 2025.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Afya ya Gaza, zaidi ya watu 880 wameuawa na wengine 2,645 kujeruhiwa katika mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni tangu makubaliano ya kusitisha vita yalipotangazwa tarehe 10 Oktoba.

Makubaliano hayo yalilenga kukomesha vita vya utawala huo wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Gazai, ambavyo vimesababisha maafa makubwa kwa kuwaua zaidi ya watu 72,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kujeruhi zaidi ya watu 172,000. Aidha, hujuma hizo zimesababisha uharibifu mkubwa uliogusa takriban asilimia 90 ya miundombinu ya kiraia tangu mwezi Oktoba 2023.

Ikiwa leo ni sikukuu ya Eid El-Adha, Wapalestina wanaoishi katika Ukanda wa Gaza eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel hawana cha kusherehekea bali wanakumbwa na jinamizi na masaibu yaliyosababishwa na utawala huo ghasibu.

Badala ya kusherehekea sikukuu hii, watoto wa Gaza wanajihusisha na uchuuzi wa bidhaa ndogo ndogo ili waweze kukimu familia zao. Eid ul Adha, inawadia huku Ukanda wa Gaza ukiendelea kuteseka kutokana na madhara ya vita na kuporomoka kwa uchumi baada ya vita vya mauaji ya kimbari vilivyoanzishwa na utawala wa Israel dhidi ya eneo hilo Oktoba 2023.

Tunamuomba Allah (SWT) awalipe malipo mema mashahidi wa njia ya haki na awape subira na nusra wafiwa na wananchi madhulumu wa Palestina. Amin.

3497621/

Habari zinazohusiana
captcha