IQNA

Uandishi wa nakala ya kipekee ya Nahj al‑Balagha waanza Najaf

15:48 - June 14, 2026
Habari ID: 3482360
IQNA – Haram tukufu ya Imam Ali (A.S.) mjini Najaf, Iraq, imetangaza kuanza kwa mradi wa kuandika nakala adhimu na ya kifahari ya kitabu cha Nahj al‑Balagha, mradi unaotajwa kuwa wa kwanza wa aina yake katika ulimwengu wa Kiislamu.

Idara ya Masuala ya Kiutamaduni na Kielimu ya Ataba (usimamizi wa haram) ya Imam Ali (A.S.), chini ya uangalizi wa Sayyid Issa Al‑Khursan, msimamizi wa haram hiyo tukufu, imeanza kutekeleza mradi huo wa kuandika nakala maalumu na yenye thamani kubwa ya Nahj al‑Balagha.

Katika mahojiano na Kituo cha Habari cha Ataba, mkuu wa idara hiyo, Karrar Jasib, alisema Nahj al‑Balagha ni hazina ya thamani kubwa iliyopokewa kutoka kwa Amiri wa Waumini, Imam Ali (A.S.).

Alieleza kuwa mradi huu ni sehemu ya mfululizo wa kazi maalumu na machapisho yanayochanganya uhalisia wa sanaa ya Kiislamu na mahitaji pamoja na ladha ya wasomaji wa zama za sasa.

Jasib aliongeza: “Toleo hili jipya ni mradi wa kipekee na usio na mfano ambao haujawahi kufanywa hapo awali kwa kiwango hiki cha mpangilio, umakini na uangalifu.”

Alibainisha pia kuwa Ataba ya Imam Ali (A.S.) katika miaka iliyopita imetoa huduma nyingi kwa kitabu cha Nahj al‑Balagha, ikiwa ni pamoja na kazi za uandishi, utafiti na maandalizi ya faharasa maalumu za kitaaluma.

Alisisitiza kuwa lengo la mradi huu ni kuwasilisha toleo la kifahari ambalo, pamoja na kuendana na ladha ya kisasa, linahifadhi pia uhalisia na urithi wa Kiislamu.

Kwa mujibu wake, hili ndilo toleo la kwanza linaloandaliwa chini ya usimamizi na uangalizi wa moja kwa moja wa Ataba ya Imam Ali (A.S.).

Kwa upande wake, msanii wa khati wa Ataba, Hazem Al‑Helou, alisema mradi huu utatumia mbinu asilia na za jadi katika uandishi wa miswada adhimu.

Alifafanua kuwa karatasi, wino, kalamu na mapambo yote yamechaguliwa kutoka katika vifaa vya asili na maalumu ili yaendane na shule za khati na mila za kale zilizotumiwa katika uandishi wa Qur’ani Tukufu na miswada mingine ya kifahari.

Alieleza kuwa utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuchukua takribani mwaka mmoja, huku kundi la wabobezi wa khati mashuhuri wa Ataba wakishiriki katika kazi hiyo.

“Kazi hii itapangwa katika juzuu tatu, kwa kufuata mtindo wa miswada ya kale iliyokusanywa kwa mujibu wa shule mashuhuri za khati,” alisema.

Aliongeza kuwa kila ukurasa utakuwa na mistari 14, idadi iliyochaguliwa kwa nia ya kubarikiwa kwa majina ya Ma’sumin kumi na wanne (A.S.).

Nahj al‑Balagha inachukuliwa kuwa mojawapo ya vyanzo muhimu zaidi vya fikra, fasihi na maarifa katika urithi wa Kiislamu, na inajumuisha khutba, barua na hekima za Amiri wa Waumini, Imam Ali (A.S.).

/3497829

captcha