IQNA

Baba na Mwanae Wamisri miongoni mwa washindi wa Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Al Ameed nchini Iraq

19:00 - June 16, 2026
Habari ID: 3482368
Amr Al Laithi Qari wa Misri katika mashindano ya Qur'ani Iraq
IQNA – Baba na mwanae kutoka Misri waliokuwa washiriki katika Tuzo ya Qur’ani ya Al Ameed nchini Iraq wamekuwa miongoni mwa waliopata nafasi za juu katika shindano hilo la kimataifa la usomaji wa Qur’ani.

Wawili hao walizungumzia mafanikio yao walipojitokeza katika kipindi cha televisheni cha mtandao wa satelaiti wa Al‑Hayat.

Mtangazaji mashuhuri wa Misri na mwanaharakati wa vyombo vya habari, Amr Al‑Laithi, alimhoji Sheikh Ezzat Rashed pamoja na mwanawe, al‑Sayed, kufuatia mafanikio yao makubwa.

Katika kipindi hicho, baba na mwana walikuwa na tilawa ya kupendeza ya Qur’ani Tukufu iliyopokelewa kwa furaha na watazamaji, huku ikidhihirisha uzuri wa sauti na hali ya kiroho katika usomaji wao.

Tilawa hiyo ilionesha pia uhusiano wa karibu kati ya baba na mwana katika safari yao ya kuhudumia Qur’ani Tukufu.

Al‑Sayed, mwenye umri wa miaka 12, alisema tayari amehifadhi juzuu 20 za Qur’ani na anaona ni fahari kubwa kutunukiwa cheo cha “Qari Kinara wa Dunia” baada ya kushinda katika Mashindano ya kimataifa ya Qur’ani ya Al‑Ameed nchini Iraq.

“Nilifurahi sana kupokea cheo hiki. Jambo la kwanza nililotamka baada ya ushindi lilikuwa jina la nchi yangu, Misri, na hilo lilinifurahisha zaidi kuliko kitu chochote,” alisema.

Qari huyo mchanga wa Misri alibainisha kuwa hii ilikuwa mara yake ya kwanza kupata cheo hicho.

Kwa upande wake, Sheikh Ezzat Rashed alieleza kwamba mwaka uliopita alishiriki katika kitengo cha watu wazima katika shindano hilo, huku mwanawe akishiriki mwaka huu katika kitengo cha vijana.

Alisisitiza kuwa ushindi wao ni fahari kwa familia yao na kwa watu wote wa Misri.

“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hii. Nilishinda mwaka uliopita na mwaka huu mwanangu ameshinda; hii ni baraka kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu,” alisema.

Mashindano ya usomaji wa  Qur’ani ya Al‑Ameed hufanyika kila mwaka kama moja ya mipango ya Haram Tukufu ya Hazrat Abbas (AS) mjini Karbala, likiwa na lengo la kueneza utamaduni wa Qur’ani Tukufu na kuhimiza Qur’ani kuwa mwongozo madhubuti kwa mtu binafsi na jamii.

/3497849

captcha