IQNA

14:45 - August 13, 2026
Habari ID: 3482620

Mafundisho ya Imamu Ridha (AS) Yaliweka Misingi ya Ustaarabu

IQNA – Urithi wa Imamu Ridha (A.S.) ni kielelezo kikamilifu cha kuonesha ukuu wa urithi wa Ahlu-Bayt (AS) wa Mtume Muhammad  (SAW), amesema msomi wa Iraq.

IMAM RIDHA AS

 

Ni turathi hai ambalo limesaidia kuhifadhi uhalisi wa utamaduni wa Kiislamu na kuweka misingi ya ustaarabu kwa vizazi vijavyo, aliandika Sadisa Halawi Hamoud, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Wasit nchini Iraq, katika makala ambayo ni kama ifuatavyo:

Imamu Ridha (AS) aliishi katika kipindi ambacho Ummah wa Kiislamu ulikuwa ukipokea turathi la mataifa ambayo yalikuwa yameingia katika ulimwengu wa Kiislamu hivi karibuni na yalikuwa yakichangia ujenzi wa ustaarabu wa Kiislamu. Uwazi huu wa kiutamaduni ulifikia kilele chake katika enzi zake; na kama wale wanaojali uhalisi wa utamaduni wa Kiislamu hawangeukabili kwa njia yoyote ile, utamaduni wa Kiislamu ungekabiliwa na hatari ya kufutika ndani ya tamaduni za kigeni.

Imamu Ridha (AS) aliielewa vyema hatari hii na akaikabili kwa uthabiti. Alilea kizazi cha wanazuoni waliokuwa walinzi wa turathi la Kiislamu; wale waliochukua jukumu la kueneza fikra sahihi ya Kiislamu kotekote katika ulimwengu wa Kiislamu, na wakalea vizazi vya kuifikisha ujumbe huu kwa ulimwengu wote.

Matokeo ya juhudi hii yalikuwa kuanzishwa kwa shule hai na yenye nguvu huko Khorasan; shule iliyojumuisha wanazuoni na wasomi wenye mwelekeo wa kipekee wa kimisheni na uenezaji wa mafundisho ya dini. Shule hii inachukuliwa kuwa sehemu ya urithi hai wa Imam Ridha (AS), na ni miongoni mwa vipengele vya pekee vya urithi wake mpana na wenye thamani.

Kwa mujibu wa vyanzo vilivyopo, idadi ya wapokezi wa hadithi za Imam Ridha (AS) inatajwa kuwa kati ya 319 na 367. Watu hao walikuwa wanafunzi wa shule hiyo na wahitimu wake. Mwandishi wa kitabu Musnad al-Imam al-Ridha — Sheikh Azizullah Attari, aliyekusanya Hadithi za Imam Ridha (AS) — ameichukulia idadi hiyo kuwa 319, na amemfafanua kila mmoja kwa ufupi, kwa kutegemea yaliyotajwa katika mfululizo wa hadithi za Musnad. Sheikh Tusi amewataja maswahaba 315 wa Imam (AS), huku Sheikh Baqir Sharif Qureshi, mwanazuoni wa Kishia kutoka Iraq, akitaja idadi yao kuwa 367.

Kuichunguza kwa ufupi Musnad al-Imam al-Ridha kunatoa taswira ya jumla kuhusu mielekeo ya shule ya Imam huyo, pamoja na sifa za kielimu na kimaadili za zama zake. Aidha, kitabu hicho kinaonesha maandalizi ya pekee yaliyofanywa na Maimamu wa Ahl al-Bayt (AS) kwa ajili ya mustakabali wa karibu na wa mbali. Mtu anayezitafakari kwa pamoja riwaya na matini zote zilizotolewa na Maimamu hao, pamoja na mwongozo wao kuelekea upeo ang’avu uliokuwa ukiwasubiri wafuasi wa Ahl al-Bayt (AS), ataelewa vyema utayari huo.

Shughuli za kielimu za Mashia zilstawi katika kipindi hiki, hali iliyojitokeza kupitia wingi wa uandishi, uhifadhi wa maandiko, ufundishaji, na usimulizi; shughuli ambazo zilienea katika nyanja zote za maarifa zilizokuwa zikijulikana wakati huo. Idadi ya Mafakihi na wapokezi waliofungamana na shule ya Ahl al-Bayt (AS) na hata madhehebu mengine ya Kiislamu iliongezeka kwa kiasi kikubwa; jambo ambalo linaonekana wazi katika maeneo mengi kwenye orodha ya wapokezi wa hadithi za Imam Ridha (AS).

Orodha hii inaonyesha shauku yao kubwa ya kupata maarifa kutoka katika shule ya Imam Ridha (AS), shule iliyokuwa na mwelekeo madhubuti wa kuhubiri katika zama zao. Hii inasisitizwa zaidi tukizingatia utofauti wa viwango vyao vya kielimu, utofauti wa maeneo yao ya asili, na tofauti za maslahi yao ya kitaaluma, jambo ambalo linabainika wazi kupitia utofauti wa maswali na mada za hadithi zilizosimuliwa kutoka kwao.

Hadithi za Imam Ridha (AS) pia zimesimuliwa na baadhi ya wanafunzi wa babu yake mkuu, Imam Sadiq (AS), baadhi ya wanafunzi wa baba yake, Imam Musa al-Kadhim (AS), na kundi la wanazuoni wa zama zake. Wasifu wa maswahaba wake muhimu zaidi na wapokezi wa Hadithi hizo unapatikana kwa ajili ya watafiti, kwani kwa maoni yetu, wasifu huu unachukuliwa kuwa nyenzo muhimu ya kukamilisha utafiti kuhusu shule ya Imam Ali ibn Musa al-Ridha (AS). Vilevile, unafunua kipengele muhimu cha maisha yake ya kielimu na ushawishi wake mkubwa wa kiakili na kistaarabu katika ulimwengu wa Kiislamu, hususan katika maeneo ya Mashariki ya Kiislamu.

Kati ya kazi muhimu zaidi za Imam Ridha (AS) ni risala tukufu ya “Sahifa al-Ridha”, ambayo kundi la wanariwaya wameliita “Musnad al-Imam al-Rida”. Jina hili linakaribiana zaidi na hadhi ya juu ya kitabu hiki, kwa sababu lina utajiri wa hadithi ambazo Imam (AS) amezisimulia kutoka kwa babu yake Mtukufu Nabii (SAW) na kutoka kwa mababu zake wapendwa wa Ahl-ul-Bayt (AS). Kundi la watafiti wametilia mkazo kuhusisha risala hii kwa Imam Ridha (AS).

Kwa vyovyote vile, kazi hii ni hazina kati ya hazina za unabii na urithi mtukufu wa Ahl-ul-Bayt (AS), na kwa upande wa mnyororo wake wa usimulizi (isnad), umefikia kilele cha heshima na utukufu.

Urithi wa Imam Ridha (AS) ni kielelezo kamili cha kuonyesha ukuu wa urithi wa Ahl-ul-Bayt (AS) na wingi wa malengo yake ya kiakili na kisayansi; urithi ulio hai ambao umesaidia kuhifadhi usahihi wa utamaduni wa Kiislamu na kuweka msingi wa ustaarabu kwa vizazi vijavyo.

3498628

Habari zinazohusiana
Kishikizo: imam ridha as
captcha