IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu: Maendeleo ya kijeshi na kielimu ya Iran yataharakishwa zaidi

17:46 - July 26, 2025
Habari ID: 3481003
IQNA – Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yameshindwa kutimiza malengo waliyojiwekea, huku akisisitiza kwamba taifa hilo litaendelea kusonga mbele kwa kasi zaidi katika nyanja za kijeshi na kielimu kwa azma iliyo imara.

Nakala ya ujumbe huo wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu inasomeka kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

Enyi wananchi wenye kuheshimika wa Iran!

Arubaini ya kuuawa shahidi wananchi wenzetu wapendwa kadhaa, ambao miongoni mwao walikuwemo makamanda waliokomaa wa kijeshi na wanasayansi watajika wa nyuklia, imewadia. Pigo hili lilitolewa na kundi khabithi na la watendajinai la utawala wa Kizayuni, ambalo ni adui muovu na mwenye kinyongo na taifa la Iran. Bila ya shaka kupoteza makamanda kama vile Mashahidi Bagheri, Salami, Rashid, Hajizadeh, Shadmani, na wanajeshi wengine, na wanasayansi kama vile Mashahidi Tehranchi na Abbasi, na wanasayansi wengine, ni jambo zito kwa taifa lolote lile. Lakini adui mpumbavu na mwenye uono finyu hakufikia lengo lake. InshaaLlah, wakati ujao utakuja kuonyesha jinsi harakati zote mbili za kijeshi na za kisayansi zitavyopiga hatua mbele kwa kasi zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma kuelekea upeo wa juu.

Mashahidi wetu walikuwa wameshachagua njia yao ambayo ni ya tamanio la kufikia daraja ya juu ya kufa Shahidi, na hatimaye walikifikia kile wanachokitamani wale wote wanaojitoa mhanga; ni hongera kwao wao; lakini msiba wake ni mgumu, mchungu, na mzito kwa taifa la Iran, hususan kwa familia za Mashahidi, na hasahasa kwa wale waliowafahamu kwa karibu.

Katika tukio hili, kuna nukta zing'arazo pia zinazoweza kuonekana kwa uwazi. Kwanza ni uvumilivu, subira, na moyo imara wa jamaa zao, ambao ni wa aina yake usioonekana isipokuwa katika matukio ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Pili, ni istiqama na uthabiti wa vyombo vilivyokuwa vikiongozwa na Mashahidi hao, ambavyo havikuruhusu pigo hili zito livizuie kutumia fursa na kuvikwamisha katika kuendeleza harakati. Na tatu ni adhama ya subira ya kimiujiza ya wananchi wa Iran, ambao walijitokeza kwa umoja wao, kwa uimara wa kiroho, na kwa azma thabiti ya kusimama kidete katika medani. Katika tukio hili, Iran ya Kiislamu kwa mara nyingine tena imedhihirisha uimara wa msingi wake. Maadui wa Iran wanapinda chuma kisichopindika.

Kwa idhini ya Allah, Iran ya Kiislamu itaimarika zaidi na zaidi siku baada ya siku.

Muhimu ni kwamba sisi tusighafilike na ukweli huu na jukumu tulilonalo mabegani mwetu. Kudumisha umoja wa kitaifa ni jukumu la kila mmoja wetu. Kasi inayohitajika katika maendeleo ya sayansi na teknolojia katika sekta zote ni jukumu la wabobezi wa kisayansi. Kulinda izza na heshima ya nchi na taifa ni wajibu usio na mpaka wa makhatibu na waandishi. Kuizatiti nchi kwa nyenzo za kulinda usalama na kujitawala kitaifa ni jukumu la makamanda wa kijeshi. Umakini, ufuatiliaji, na kuleta ufanisi wa kazi za nchi ni wajibu wa vyombo vyote vya utendaji. Uongozaji wa kiroho, kuzinawirisha nyoyo, na kuwausia watu wawe na subira, utulivu, na uthabiti ni wajibu wa viongozi wa dini. Na kudumisha ari, hamasa na uelewa wa kimapinduzi ni jukumu la kila mmoja wetu, hususan vijana. Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwingi wa Rehema, awajaalie wote mafanikio.

Amani iwe juu ya taifa la Iran na amani iwe juu ya vijana Mashahidi, kwa wanawake na watoto Mashahidi, na kwa Mashahidi wote na wafiwa wao.

Amani ya Allah na Rehma Zake ziwe juu yenu

Sayyid Ali Khamenei

Chanzo: khamenei.ir

3493986

Habari zinazohusiana
captcha