IQNA

Sheikh Omar Hashem aliyekuwa Mkuu wa Al-Azhar aenziwa Tehran kwa kukuza umoja Kiislamu

10:30 - February 09, 2026
Habari ID: 3481907
IQNA – Hafla maalumu imefanyika mjini Tehran siku ya Jumapili kutoa heshima kwa marehemu mwanazuoni mashuhuri Sheikh Ahmed Omar Hashem, aliyewahi kuwa Rais wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar cha Misri.

Hafla hiyo iliandaliwa na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Madhehebu ya Kiislamu (IUID) jijini Tehran. Washiriki walisisitiza kuwa marehemu Sheikh Hashem alikuwa mwendelezaji wa njia ya wanazuoni wakubwa wa Al-Azhar, na alichukua nafasi ya kipekee katika kuimarisha ukuruba wa madhehebu ya Kiislamu na mwingiliano chanya kati ya Uislamu na ulimwengu mpana.

Rais wa IUID, Profesa Mohammad Hadi Fallahzadeh, alitoa rambirambi kwa kufuatia kifo cha mwanazuoni huyo na kusema kuwa kuondoka kwa Sheikh Ahmed Omar Hashem ni pigo kubwa kwa jumuiya ya kitaaluma na Umma wa Kiislamu kwa ujumla.

“Kwa niaba ya maprofesa na wafanyakazi wenzangu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Madhehebu ya Kiislamu, natoa pole kwa familia ya marehemu, wenzake katika Chuo Kikuu cha Al-Azhar, jamii ya Misri, wasomi na Waislamu wote, hususan mgeni wetu mpendwa Mohamed Zia, mkuu wa Ofisi ya Kulinda Maslahi ya Misri nchini Iran,” alisema.

Aliongeza kuwa, “Leo tumekusanyika kuuenzi msafara mzima wa juhudi za kielimu na kidini, na kumuenzi shakhsia mkubwa kutoka ulimwengu wa Kiislamu; mwanazuoni mchamungu, mrekebishaji mwenye huruma, msomi mahiri, na bingwa wa elimu ya Hadithi, ambaye kumbukumbu yake yenye baraka ni kielelezo cha heshima kwa elimu, vitendo na jitihada zisizochoka katika njia ya Uislamu safi wa Muhammadiyya, pamoja na kueneza utamaduni wa wastani na mazungumzo yenye kujenga.”

Akiashiria hadhi ya Chuo Kikuu cha Al-Azhar, Fallahzadeh alisema kuwa Al-Azhar, kama chuo kikuu cha zamani zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu, daima kimekuwa bendera ya elimu za dini, ngome ya mantiki, na nguzo imara dhidi ya misimamo mikali.

“Katika kipindi cha uongozi na shughuli zake za kielimu, Sheikh Ahmed Omar Hashem alichangia kwa namna ya pekee katika kueneza Uislamu wa rehema, kusogeza karibu madhehebu ya Kiislamu, na kuimarisha mawasiliano yenye kujenga na ulimwengu.”

Aliendelea kusema, “Alikuwa mwendelezo wa njia ya wanazuoni wa Al-Azhar, wanazuoni waliotilia mkazo daima nafasi ya elimu na wanazuoni katika kutatua migogoro, kutoa mwanga dhidi ya upotoshaji, na kuwasilisha ufahamu thabiti na wa wastani wa dini.”

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alizungumzia dhamira ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Madhehebu ya Kiislamu, akibainisha kuwa chuo hicho kilianzishwa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa misingi ya fikra za kimsingi za Imam Khomeini (RA), na kimeendelea na njia hiyo kwa msaada na uongozi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Dhamira hiyo inajikita katika mazungumzo baina ya madhehebu ya Kiislamu, ulinganishi wa dini na madhehebu, pamoja na kukabiliana kielimu na mikondo ya misimamo mikali na ya takfiri.

Aidha, Abbas Khameyar, aliyewahi kuwa mwambata wa masuala ya utamaduni wa Iran nchini Lebanon, alihutubia hafla hiyo kwa kuchambua maisha, fikra, misimamo, na athari za kielimu na kijamii za Sheikh Ahmed Omar Hashem.

Habari inayohusiana:

Khameyar alisema kuwa Sheikh Hashem anaweza kuhesabiwa kuwa ni kiungo muhimu katika mlolongo wa wanazuoni wa Al-Azhar, ambao kila mmoja katika zama zake amebeba jukumu la kulinda mjadala wa wastani na ukaribu wa Kiislamu.

“Kama katika zama fulani jukumu hili lilijidhihirisha kupitia ijtihadi ya kifiqhi na nadharia za kielimu, basi katika zama za sasa limeendelea kupitia mjadala wa maadili na ustaarabu,” alisema.

Aliongeza kuwa Sheikh Hashem alichukua nafasi muhimu sana katika malezi ya kizazi kipya cha wanazuoni na walimu wa Kiislamu.

“Katika kipindi chake cha uongozi na kazi za kielimu, alitoa mchango wa msingi katika kuimarisha uelewa wa wastani wa Uislamu ndani ya mitaala na programu za elimu, madarasa, mihadhara, na vyombo vya habari vinavyohusiana na Al-Azhar.”

Kwa upande wake, Mohammad Zia, mkuu wa Ofisi ya Kulinda Maslahi ya Misri nchini Iran, alisema katika hotuba yake kuwa marehemu Sheikh Ahmed Omar Hashem alikuwa shakhsia mashuhuri katika fikra za Kiislamu za zama hizi, na ishara ya mantiki, wastani, na mwangaza wa kidini, aliyetoa mchango wenye athari katika kulinda uelewa wa dini na kupambana na misimamo mikali.

Zia amesisitiza kuwa hafla hiyo ya kumbukumbu si sherehe ya kumuenzi msomi mmoja pekee, bali ni kutambua nafasi na wajibu wa wanazuoni wa dini katika kuongoza jamii, kuunda ufahamu wa umma, na kusimamisha misingi ya wastani, busara, na hekima katika ulimwengu wa Kiislamu.

Aliongeza kuwa kufanyika kwa hafla hiyo mjini Tehran kunabeba ujumbe muhimu katika kuimarisha mazungumzo ya kitamaduni na kielimu kati ya nchi za Kiislamu, na kunaashiria uwezo mkubwa uliopo wa kukuza maelewano, ushirikiano wa kielimu, na mwingiliano wa kitaaluma baina ya mataifa ya Kiislamu.

4333226

Habari zinazohusiana
captcha