IQNA

Kiongozi wa Hizbullah akumbusha kuhusu jinai za Saddam dhidi ya wafanyaziara wa 'Arubaini'

16:20 - October 08, 2020
Habari ID: 3473240
TEHRAN (IQNA)- Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amezungumza katika mkesha wa Siku ya Arubaini ya Imam Hussein AS na kukumbusha kuhusu jinai za mtawala wa zamani wa Iraq, Saddam, dhidi ya wafanyaziara wa Siku ya Arubaini.

Siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu, ilifanyika majlisi ya kwanza ya siku ya Arubaini (Arbaeen, Arobaini) tangu kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW Imam Hussein bin Ali AS na watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume ambao waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria.

Katika mkesha wa siku hii, Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ametoa hotuba muhimu na kusema: "Siku hii imekuwa ikiadhimishwa katika kipindi chote cha historia lakini katika zama hizi, utawala wa dikteta Saddam ulianza kuzuia maadhimisho ya Siku ya Arubaini na kuwapiga marufuku Waislamu wa madhehebu ya Shia kushiriki katika matembezi ya siku hii. Hata baadhi ya miaka, utawala  huo, ambao hatimaye ulipinduliwa, ulitumia ndege za kivita na helikopta kuwalenga wafanyaziara wa Imam Hussein AS.

Aidha amesema kuwa, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran umeleta mabadiliko makubwa katika eneo hili na umeandaa mazingira ya kufanyika kwa ufanisi mkubwa Arubaini ya Imam Husain AS.

Sayyid Hassan Nasrullah aidha amesema, matembezi makubwa ya mamilioni ya maashiki wa Ahlul Bayt AS wakati wa kumbukumbu za 40 ya Imam Husain AS ni tukio kubwa sana linaloshuhudiwa katika zama hizi. Amesema, harakati ya mwamko wa Kiislamu na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran pamoja na kupinduliwa utawala wa kidikteta wa Saddam kumewafungulia milango mamilioni ya  wananchi wa Iraq na mamilioni ya wapenzi wa Ahlul Baiyt kutoka nje ya Iraq kufanya ziara kwa ufanisi mkubwa katika Haram ya Imam Husain AS huko Karbala.

Amesema, mataifa ya dunia yanapoona kwenye vioo vya televisheni, mamilioni ya watu wanajitokeza kufanya ziara ya Arubaini ya Imam Husain AS, huzidi kupata mwamko na welewa wa malengo ya mtukufu huyo na mapambano yake katika jangwa la Karbala mwaka 61 Hijria.

3928032

captcha