IQNA

16:29 - October 08, 2020
News ID: 3473241
TEHRAN (IQNA) - Wairaki zaidi ya milioni moja wamewasili katika Haram ya Imam Husain AS huko Karbala kuwawakilisha mamilioni ya wapenzi wa Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad SAW ambao mwaka huu wameshindwa kwenda Iraq kushiriki kumbukumbu hizo kutokana na corona.

Baada ya kutembea kwa miguu kwa mamia ya kilomita, kundi la mwisho la maashiki wa Imam Husain AS liliwasili Karbala jana Jumatano kwa ajili ya maadhimisho yaliyofana ya 40 ya Imam Husain AS.

Kama tunavyojua, idadi kubwa ya Waislamu na wafuasi wa dini nyinginezo kwa miaka mingi huwa wanatembea kwa miguu ambako ni maarufu kwa jina la Mashaya, kutoka mji wa Najaf kwa ajili ya kwenda kufanya ziara katika Haram na bwana huyo wa mashahidi huko Karbala katika maadhimisho ya 40 ya Imam Husain AS.

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa, mwaka jana zaidi ya wafanya ziara milioni 18 walishiriki katika matembezi hayo ya Arubaini ya Imam Husain AS, matembezi ambayo yanahesabiwa kuwa ni mjumuiko mkubwa zaidi wa kidini wa kila mwaka duniani. Taarifa zinasema kuwa, wafanya ziara kutoka nchi 80 duniani hushiriki katika matembezi hayo ya kimaanawi yanayoshirikisha wazee kwa vijana, wanawake kwa wanaume, wakubwa kwa wadogo.

Mwaka huu matembezi hayo yamefanywa na mamilioni ya maashiki wa Imam Husain AS wa kona zote za Iraq tu bila ya kushirikisha wafanya ziara kutoka nje ya nchi hiyo kutokana na maambukizi ya kirusi cha corona. 

Siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamariya, ilifanyika majlisi ya kwanza ya siku ya Arubaini tangu kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) Imam Hussein bin Ali AS na watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume ambao waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria. Majlisi ya siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume na masahaba zake watiifu ambao walijisabilia roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika ardhi ya Karbala. Katika siku hii ya Arubaini pia msafara wa mateka wa Ahlul-Baiti wa Mtume uliokuwa umepelekwa Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiyah uliwasili Karbala ukiwa na kichwa cha Imam Hussein na kukutana hapo na Sahaba wa Mtume, Jabir bin Abdillah al Ansari na wafuasi wengine wa Imam waliokwenda hapo kufanya ziara. Siku hiyo kichwa cha Imam Hussein kilizikwa pamoja na mwili wake. 

 

 
 

3928063

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: