IQNA

Tuzo ya Sira ya Mtume yazinduliwa Algeria kwa heshima ya Maulidi ya Mtume Muhammad (SAW)

15:22 - September 07, 2025
Habari ID: 3481195
IQNA-Wizara ya Mambo ya Dini na Wakfu nchini Algeria imetangaza kuanzishwa kwa mashindano ya kimataifa kuhusu Sira au mfumo wa maisha ya Mtume Muhammad (SAW) kwa muktadha wa kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume huyo wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu.

Tukio hili limepewa jina rasmi la Tuzo ya Algeria kwa Sira ya Mtume (SAW), na linakusudia kuimarisha maadili ya kiroho na kibinadamu yanayotokana na maisha ya Mtume, sambamba na kuhamasisha utafiti wa kielimu na ubunifu wa kiakili kwa ajili ya kuhifadhi na kuendeleza urithi wake mtukufu.

Katika taarifa rasmi, wizara hiyo imeeleza kuwa tuzo hii ni ishara ya dhamira ya serikali ya Algeria kuinua hadhi ya Sira ya Mtume Muhammad (SAW) na kueneza athari zake za kielimu na kitamaduni. Kwa kufanya hivyo, inasaidia kuimarisha maadili ya kiutu na kiakhlaqi yaliyodhihirishwa na Mtume (SAW), na kuyasambaza kwa vizazi vya sasa na vijavyo ili yawe mwongozo wa kukabiliana na changamoto za kisasa.

15:22 - 2025/09/07

Serikali ya Algeria imeeleza kuwa kuingizwa kwa mpango huu katika ajenda ya kitaifa ni ushahidi wa imani yao thabiti juu ya umuhimu wa dini kama nguzo ya usalama wa taifa. Kupitia kuimarisha utambulisho wa kidini na mshikamano wa kitaifa, pamoja na kupambana na misimamo mikali kwa kutumia mtazamo wa wastani uliochochewa na maisha ya Mtume (SAW), tuzo hii inachukua nafasi ya kipekee katika mkakati wa kitaifa.

Mashindano haya ya kwanza yalizinduliwa baada ya ufunguzi wa Msikiti Mkuu wa Algiers, ambao unachukuliwa kuwa miongoni mwa alama kuu za kidini na kitamaduni katika Algeria na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.

Kwa mujibu wa madhehebu tofauti, tarehe ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) huadhimishwa kwa nyakati tofauti: Waislamu wa Kishia huamini kuwa ni tarehe 17 ya mwezi wa Rabi al-Awwal (Septemba 10 mwaka huu), ilhali Waislamu wa Kisunni huadhimisha tarehe 12 ya mwezi huo (Septemba 5) kama siku ya kuzaliwa kwa Mtume (SAW).

3494493

captcha