IQNA

Kiongozi wa Ansarullah akosoa ukimya wa Umma wa Kiislamu kuhusu mauaji ya kimbari Gaza

20:19 - May 09, 2025
Habari ID: 3480658
IQNA-Sayyid Abdul-Malik Badr al-Din al-Houthi, Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameeleza kuwa, jamii za Kiarabu na Umma wa Kiislamu zinabeba dhima ya msingi kuhusu mauaji ya kimbari yanayoendelea kutekelezwa na utawala dhalimu wa Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza akisisitiza matokeo mabaya ya kutochukua kwao hatua.

Al-Houthi amelaani mauaji yanayoendelea Gaza, na kuyataja kuwa "uhalifu wa karne." Kiongozi huyo wa Ansarullah ya Yemen ameonyesha masikitiko makubwa kutokana na mwitikio hasi wa mamilioni ya Waislamu kwa ukatili wa kila siku unaowakabili watu wa Palestina. Matamshi ya Al-Houthi ni kilio cha hadharnia kwa Ummah wa Kiislamu kuamka katika majukumu yao na kuchukua msimamo dhidi ya dhulma.

Al-Houthi amesisitiza kuwa, adui anaendeleza mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya Gaza kwa muda wa mwezi wa kumi na tisa mfululizo hukuu dunia ikishindwa kuchukuua hatua za maana kusitisha jinai za Israel.

Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesikitishwa na uzembe wa Waarabu na Waislamu katika majukumu yao matukufu yakiwemo ya jihadi na kusimama dhidi ya dhulma.

Ameonya kwamba kupuuza matukio haya hakutauepusha Umma na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na kwamba, ukimya huu utakuwa na matokeo mabaya mbele ya Mwenyezi Mungu. Aidha ameashiria kuwa, utawala wa Kizayuni unayalenga mataifa yote na kutaka kuyaangamiza kabisa huku akiwataka Waislamu kutambua tishio la pamoja na kuungana dhidi yake.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, asasi mbalimbali za kimataifa zimeendelea kuonya kuhusiana na hali mbaya ya uhaba na ukosefu wa chakula katika Ukanda wa Gaza na kueleza kuwa, hivi sasa maghala ya chakula katika ukanda huo yapo tupu.

Utawala katili wa Israel ulianzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7 2023, kama jibu kwa operesheni ya kihistoria ya kulipiza kisasi wapigania ukombozi wa Palestina. Tokea wakati huo Isael imeua Wapalestina zaidi ya 52,700, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Wakati huohuo, utawala huo umeshadidisha  mzingiro wake ulioanza mwaka 2007 dhidi ya Gaza.

Jeshi la Yemen limekuwa likitekeleza operesheni za kulipiza kisasi kwa niaba ya Wapalestina Gaza na kuweka mzingiro wa baharini dhidi ya meli na vyombo vya majini vya Israel vinavyoelekea katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu tangu Oktoba 2023.

4281160

Habari zinazohusiana
captcha