IQNA

Uturuki yapunguza makali ya sheria za kuzuia COVID-19 misikitini

20:19 - November 13, 2021
Habari ID: 3474553
TEHRAN (IQNA)- Wakuu wa Uturuki wameamua kupunguza makali ya sheria ambazo zinatumika misikitini katika wakati huu wa janga la COVID-19.

Kwa mujibu wa taarifa, Idara ya Masuala ya Kidini Katika Ofisi ya Rais wa Uturuki (Diyanet), imeondoa sheria za waumini kutokaribiana ndani ya misikiti ambayo imekuwa ikitumiak tokea mwaka jana. Uamuzi huo umechukuliwa baada ya maambukizi ya COVID-19 kupungua kwa kiasi kikubwa.

Mwenyekiti wa Diyanet Ali Erbas amewatumia mamufti wote ujumbe Ijumaa akisema Sala sasa isaliwe katika safu za kawaida kwa mujibu wa Fiqhi ya Kiislamu. Hatahivyo ametoa wito kwa waumini kuendelea kuzingatia kanunu za kiafya ikiwa ni pamoja na kuendelea kuvaa barakoa wakati wa Sala.

Uturuki ilifunga misikiti wakati wa siku za mwanzo za janga la COVID-19 lakini misikiti hiyo ilifunguliwa tena Mei 2020 kwa sharti kuwa waumini wasikaribiane wakati wa Sala. Misikiti imekuwa ikijaa hadi barabarani wakati wa Sala ya Ijumaa kutokana na kuzingatiwa sheria ya kutokaribiana.

Erbas amesema hakuna tatizo kubwa katika misikiti sasa kwani waumini wamekuwa wakifuata maagizo ya wakuu wa afya kuhusu COVID-19. Aidha amesema idadi kubwa ya watu wamepata chanjo ya COVID-19 hivyo hatari ya maambukizi imepungua.

/3476451/

captcha