IQNA

Kadhia ya Palestina

Utawala wa Kizayuni wafuta mpango wa kuwazuia Waislamu kuingia Msikiti wa Al-Aqsa katika Mwezi wa Ramadhani

18:18 - March 06, 2024
Habari ID: 3478461
IQNA - Utawala wa Kizayuni wa Israel unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina umetangaza siku ya Jumanne kwamba utawaruhusu waumini kuingia katika Msikiti wa al-Aqsa katika eneo la Quds (Jerusalem) katika wiki ya kwanza ya mwezi wa Ramadhani, na hivyo kutupilia mbali mpango wa awali wa kuweka vizuizi.

Uamuzi huo umekuja baada ya makundi ya wapigania ukombozi wa Palestina kuuonya utawala huo dhidi ya kuweka vikwazo vyovyote kwenye eneo hilo takatifu. Wakati huo huo, Marekani pia imeutaka utawala ghasibu wa Israel kuwaruhusu Waislamu kutekeleza ibada katika msikiti huo mtakatifu  wa mwezi wa Ramadhani.

"Kila wiki tathmini ya usalama itafanywa na uamuzi utachukuliwa ipasavyo," ofisi ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ilitangaza katika taarifa ya Jumanne.

Waziri mwenye itikadi kali wa utawala huo Itamar Ben-Gvir alikuwa amepinga kuingia kwa Waislamu Wapalestina kutoka Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu kwenda al-Quds kuswali wakati wa mwezi wa Ramadhani, licha ya onyo kutoka kwa mashirika ya kijasusi wa Israel kwamba hatua hiyo inaweza kuzusha ghasia.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, Ismail Haniyah, alikuwa ametoa wito wa kuwepo kwa vuguvugu kubwa kuhusu al-Aqsa kwa ajili ya kuanza kwa Ramadhani.

Ismail Haniyah amesema katika ujumbe wa televisheni kwamba: "Kuzingirwa kwa Msikiti wa Al-Aqsa na kuzingirwa kwa Ukanda wa Gaza ni kitu kimoja." 

Haniyeh alikuwa akijibu tangazo lililotolewa na utawala wa Israel kwamba utaweka vizuizi vya kuingia Msikiti wa Al-Aqsa katika Mji Mkongwe wa al-Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu wakati wa mfungo wa Ramadhani eti kulingana na "mahitaji ya usalama."

Siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka huu inasadifiana na Machi 11 au 12.

Makundi kadhaa ya wapigania ukombozi wa Palestina yametoa wito kwa watetezi wa haki kote ulimwenguni kujiunga na kampeni ya kimataifa iliyopewa jina la "Kimbunga cha Ramadhani.

Kampeni hiyo inajumuisha maandamano katika sehemu mbalimbali za dunia wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa mshikamano na Gaza na Palestina.

Utawala wa Israel ulianzisha vita vya mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7 na hadi sasa vita hivyo vya mauaji ya kimbari vimepelekea kuuawa Wapalestina wasiopungua 30,410, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na wengine 71,700 kujeruhiwa.

Pia kumetokea uharibifu mkubwa, huku karibu wakazi wote karibu milioni mbili wa Gaza wakilazimika  kuyahama makazi yao. Aidha njaa imeenea kote katika eneo hilo kutokana na vita na mzingiro wa utawala wa Israel.

Katika taarifa siku ya Jumapili, makundi ya Wapalestina yalitoa wito kwa watu kushiriki katika kampeni ya ‘Kimbunga cha Ramadhani' katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

3487449

Habari zinazohusiana
captcha