IQNA

Jinai ya Israel

Hamas yathibitisha kuuawa shahidi kiongozi wake, Yahya Sinwar, katika hujuma ya kigaidi ya Israel

22:00 - October 18, 2024
Habari ID: 3479609
IQNA-Afisa mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amethibitisha kuwa kiongozi wa harakati hiyo, Yahya Sinwar, ameuawa shahidi katika shambulizi la kigaidi la jeshi katili la Israel katika mji wa Rafah huko Gaza.

Khalil al Hayya, mkuu wa Hamas huko Gaza, ametoa taarifa huyo leo Ijumaa, siku moja baada ya ripoti za kuuawa shahidi Yahya Sinwar.

Al Hayya amemtaja Yahya Sinwar kuwa alikuwa "imara, shujaa na jasiri” na kwamba alisabilia maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa watu wa Palestina.

“Sinwar ameishi maisha yake yote kama mpiganaji wa Jihadi. Tangu siku za awali za maisha yake, alikuwa akijishughulisha na mapambano kama mwanamuqawama", amesisitiza Khalil al Hayya.

Kiongozi huyo wa Hamas alinusurika majaribio mengi ya mauaji kabla na baada ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa mnamo Oktoba 7, 2023.

Sinwar, aliyekuwa na umri wa miaka 62, alikuwa na nafasi kubwa katika kuratibu na kusimamia operesheni hiyo ya kihistoria iliyoutikisa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kabla ya kuwa kiongozi wa Hamas huko Gaza mnamo 2017, Sinwar alifungwa miaka 22 katika jela ya Israel. Aliachiliwa huru kama sehemu ya ubadilishaji wa wafungwa mnamo 2011.

"Hamas kamwe haitaacha njia ya Muqawama... mapambano yetu ya yataendelea hadi Palestina yote itakapokombolewa," alisema Yahya Sinwar wakati wa hotuba yake huko Gaza mwishoni mwa Oktoba 2017.

Kauli ya Iran

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imetoa salamu za rambirambi kufuatia mauaji ya Yahya Sinwar, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Hamas.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imesisitiza kuwa, kuuawa Mujahidina wanaopigana katika njia ya heshima na utu wa binadamu, si tu kwamba hakutii dosari katika fikra na njia ya Muqawama na mapambano ya ukombozi, bali kifo chao kitukufu ni msisitizo juu ya haki na usahihi wa njia yao na kinatoa msukumo na kuwahamasisha wafuasi wa njia hiyo na Mujahidina katika njia ya kupigania izza na uhuru.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani jinai ya utawala wa Kizayuni ya kuwaua kigaidi viongozi na shakhsia wa Palestina na kutangaza kuwa, Marekani ni mshirika katika kutekeleza jinai hizo na inawajibika kwa kutoa silaha na kuuhami kifedha na kisiasa utawala huo.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa, jina la Sinwar limewekwa katika kitabu cha mashujaa wakubwa wa Umma wa Kiislamu kama Sheikh Ahmad Yassin, Abdul Aziz Rantisi, Qassem Soleimani, Ismail Haniyeh na Sayyid Hassan Nasrullah, ambao wamesabilia uhai wao wote katika njia ya Muqawama na Jihadi kwa ajili ya kukomesha uvamizi na kutimiza haki ya kisheria na halali ya kujitawala na haki ya kimsingi ya kuishi kwa heshima.

3490333

 

captcha