IQNA

Ukosoaji wa kilipu ya Akili Mnemba inayoonyesha uharibifu wa Msikiti wa Al-Aqsa

15:05 - April 20, 2025
Habari ID: 3480568
IQNA – Nchi kadhaa za Kiarabu zimelaani vikali kusambazwa kwa klipu iliyotengenezwa kwa kutumia Akili Mnemba (AI) na walowezi wa Kizayuni wa Israel, inayoonyesha uharibifu wa Msikiti wa Al-Aqsa ulioko katika al-Quds inayokaliwa kwa mabavu, na ujenzi wa hekalu la Kiyahudi mahali pake.

Video hiyo, ambayo imesambazwa na majukwaa ya Kizayuni yenye misimamo mikali, inaonyesha eneo hilo takatifu la Kiislamu likilipuliwa na kubadilishwa kuwa kile kinachoitwa Hekalu la Tatu. Pia ina ujumbe unaosema: “Mwaka Ujao (Quds) Jerusalem… Masihi Sasa.” Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imetoa taarifa ikisema kuwa waundaji na wasambazaji wa video hiyo wanahamasisha “uchochezi wa kimfumo” dhidi ya maeneo matakatifu ya Kikristo na Kiislamu katika al-Quds inayokaliwa kwa mabavu na Israel. Wizara hiyo ilizitaka jamii za kimataifa kuchukulia video hiyo kwa uzito na kuchukua hatua stahiki za kisheria na kidiplomasia.

Taarifa hiyo pia ilitaka kukomeshwa kwa sera ya serikali ya Israel ya kuwabagua na kuwatenga Wapalestina. Wizara ya Mambo ya Nje ya Jordan, kupitia shirika la habari la serikali la Petra, ililaani kitendo kuwa ni “uchochezi wa kibaguzi na wa msimamo mkali” unaofanywa na makundi ya walowezi wa Israel. Ilitaja video hiyo kama sehemu ya muktadha mpana wa kuongezeka kwa shughuli za walowezi, ikiwemo “uvamizi” na “vitendo vya uchokozi” vinavyofanyika chini ya ulinzi wa vikosi vya usalama vya Israel.

Wizara hiyo ilisisitiza kuwa Msikiti wa Al-Aqsa, ulio katika eneo la ukubwa wa dunam 144 (takriban ekari 35), ni mahali pa ibada kwa Waislamu pekee. Ilieleza pia kuwa Idara ya Wakfu ya Quds na Masuala ya Msikiti wa Al-Aqsa—chini ya Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Jordan—ndiyo mamlaka pekee yenye jukumu la kusimamia eneo hilo na kudhibiti ufikiaji wake.

Qatar pia iliungana katika kulaani tukio hilo, ikielezea video hiyo na ujumbe wake kama “uchochezi hatari” ambao unaweza kuchochea zaidi mvutano katika eneo hilo, hasa ikizingatiwa vita inayoendelea Gaza. Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar ilisisitiza msimamo wake mkali wa kupinga juhudi zozote za kubadilisha hali ya kisheria na kihistoria ya Msikiti wa Al-Aqsa au maeneo mengine ya kidini katika al-Quds. Maafisa wa Israel wamekuwa wakidai mara kwa mara kuwa hali ya sasa katika Msikiti wa Al-Aqsa inaendelea kuheshimiwa.

Hata hivyo, Idara ya Wakfu ya Kiislamu huko al-Quds inapingana na madai hayo. Idara hiyo imesisitiza kuwa hatua za hivi karibuni zinazochukuliwa na mamlaka ya Israel na walowezi ni “ukiukaji wa hali ya kipekee ya Kiislamu” ya eneo hilo usiowahi kushuhudiwa. Mpangilio wa hali ya sasa, ambao ulianzishwa kabla ya Vita vya Waarabu na Israel vya mwaka 1967, unabainisha kuwa idara hiyo ya Wakfu ndiyo inayosimamia Msikiti wa Al-Aqsa na kwamba ni Waislamu pekee wanaoruhusiwa kuswali hapo.

Wasio Waislamu wanaruhusiwa kuutembelea chini ya masharti maalum lakini hawaruhusiwi kuswali. Mvutano umeongezeka katika siku za hivi karibuni huku makundi ya mrengo wa kulia yakihamasisha watu kutembelea kwa wingi eneo hilo wakati wa sikukuu ya Kiyahudi ya Pasaka, iliyaanza Jumapili iliyopita.

Tangu mwaka 2003, mamlaka ya Israel imewaruhusu walowezi na wageni wasio Waislamu kuingia kwenye eneo hilo karibu kila siku—kitendo ambacho Wapalestina na viongozi wa Kiislamu wanakitazama kama changamoto kwa hadhi ya kihistoria ya msikiti huo. Msikiti wa Al-Aqsa, ulioko Mashariki mwa al-Quds, ni mahali patakatifu pa tatu kwa Uislamu baada ya Makka na Madina. Israel ilikalia kwa mabavu mji huo wakati wa vita vya mwaka 1967 na baadaye ikaudhibiti rasmi mwaka 1980, hatua ambayo haijatambuliwa na jumuiya kubwa ya kimataifa. 

3492754

Habari zinazohusiana
captcha